UKISOMA kitabu cha ‘I Can , I Must, I Will:The Sprit of Succes’ cha Dk.Regnald Mengi, Mwenyekiti wa IPP kila jambo linawezekana kwa kuwa na ari, dhamira ya kufikia lengo na kuthubutu.
Inawezekana kufanya chochote na kutimiza malengo hata kama kuna hofu au wasiwasi unaonekana mbele.
Serikali imedhamiria kuipa Tanzania umeme kwa namna yoyote ile ikidhamiria kuongeza umeme kutoka megawati 4,000 hadi 8,000 ifikapo 2030.
Kama Rais Samia Suluhu Hassan, anavyosema maendeleo ni lazima ni kama kupiga hatua lazima kusogea mbele kwa namna yoyote ile.
Tanzania inapoingia kwenye umeme wa nyuklia inakuwa nchi ya pili barani Afrika Kusini ndiyo pekee inayotumia umeme huo.
Inatumia urani kuzalisha umeme wa nyuklia kwenye kinu cha Koeberg, ambacho kinazalisha takriban asilimia tano ya nishati ya nchi hiyo.
Taarifa za mtandaoni zinasema na kuongeza kuwa Misri, Kenya na Nigeria ni miongoni mwa mataifa zaidi ya 20 ya Afrika yanayotafuta maendeleo ya miundombinu ya nishati ya nyuklia ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme.
Leo Tanzania nayo imo, sasa ni rasmi itaanza kuzalisha umeme wa nyuklia na kinu kitawekwa Tunduru mkoani Ruvuma.
Rais Samia analitangazia taifa wiki hii kwenye mkatano wa kampeni mkoani Ruvuma, akisema uzalishaji wa umeme wa nyuklia ni dhahiri na kinu cha kuchakata nishati hiyo kitawekwa wilayani Namtumbo.
Mgombea huyo wa urais wa CCM, anatoa hakikisho hilo akisema “Pamoja na dhamira yetu … siyo tu kuchimba na kuuza nje ya nchi bali kutumia urani kuzalisha umeme wa nguvu za nyuklia tuzalishe umeme hapa Namtumbo.”
Anaongeza kuwa serikali katika miaka mitano ijayo inakusudia kuzalisha umeme mara dufu ukiwamo wa nyuklia ifikapo mwaka 2030 na kuongeza kuwa urani itachenjuliwa na kuzalishwa umeme wa nyuklia ambayo kidunia inakubalika kama nishati safi
Ni jambo jema linaloendelea kuifungua Tanzania na kuihakikishia maendeleo kwa sababu umeme ni nguzo ya kila kitu kuanzia majumbani, kazini, viwandani, migodini , mashambani nadarasani.
Rais amedhihirisha kuwa Tanzania inaweza kutumia vyanzo vyote vya umeme , kama alivyotangaza akiwa Songwe kuwa mikakati ipo mbioni kuanza kuvuna umeme wa joto ardhi ulioko kwenye bonde la ufa mkoani humo.Ni wazi uwekezaji kwenye umeme huo ni fursa kwa vijana na wafanyabiashara wengine.
Pamoja na umeme wa urani, joto ardhi, gesi na maji upo umeme jua.
Umeme jua au sola nao ni muhimu taifa lianze kuwekeza, yote hayo ni kuongeza zaidi uzalishaji wa nishati jadidifu ambayo pia inahusisha upepo. Umeme jua ni mwingi kwa sababu karibu Tanzania nzima inapata mwanga wa jua kwa hiyo serikali inaweza kuweka ruzuku kwenye vifaa vya sola hasa paneli zitakazo wekwa kwenye mapaa.
Vifaa hivyo viwekwe juu ya mapaa ya viwanda, shule, vyuo, nyumba za ibada, hoteli, kumbi na majumbani mradi ukianzia kwenye majiji Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Mbeya Mwanza , Arusha na miji mingine mikubwa ili kuvuna umeme.
Miradi hii ya kuendeleza umemejua inatunza mazingira, inawapa vijana wengi ajira za aina mbali mbali. Kwa kuanza ni lazima wafundishwe katika vyuo vya ufundi vya ngazi mbali mbali za kitaaluma.
Aidha, wafundishwe kubuni na kujenga majengo yanayoweza kuwekewa paneli za umeme jua. Kuvifunga, pia kutengeneza baadhi ya vifaa vya ujenzi na vya sola, kufanya kazi kwenye usafirishaji wake kutoka maeneo ya uzalishaji mpaka kwa wateja.
Hongera Rais Samia unafanya mambo makubwa sekta nyingi na kwenye umeme wa nyuklia utandika historia kwa wino wa dhahabu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED