Timu zivune zilichopanda Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:25 AM Sep 15 2025
Uwanja wa mpira
Picha: Mtandao
Uwanja wa mpira

ILIKUWA ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini, hatimaye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/26 inatarajiwa kuanza kesho kutwa.

Msimu huu ligi ilichezewa kutokana na Tanzania kuwa wenyeji wenza wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa ndani nchini (CHAN) lililoanza Agosti 2 hadi 30, ikishuhudiwa kombe likielekea nchini Morocco.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, KMC na Dodoma Jiji ndizo zitakazokata utepe wa ligi hiyo, zitakapokwaana kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, saa 10:00, jioni, kabla ya saa 1:00 usiku, Uwanja wa Mkwakwani Tanga, kuwa na mchezo wa pili, kati ya Coastal Union dhidi ya Prisons.

Alhamsi kutakuwa na michezo mingine miwili, ambapo Mashujaa FC, itakuwa nyumbani, Lake Tanganyika, Kigoma, ikiikaribisha, JKT Tanzania, saa 10:15, kabla ya saa 1:00 usiku, mashabiki kushuhudia mechi nyingie kati ya Namungo, itakayokuwa nyumbani dhidi ya Pamba Jiji.

Ni mechi ambazo kila timu itakuwa inajitahidi kuonyesha kile ambacho ilikuwa ikikifanya kwenye maandalizi ya msimu 'pre season'.

Kwa bahati nzuri timu zote msimu huu zimepata 'pre season' ndefu ya zaidi ya wiki sita, kutokana na kwani hata wakati fainali za CHAN zilipokuwa zinaendelea zenyewe zilikuwa kwenye maandalizi.

Hatutarajii tena makocha kuanza kulalamika kuwa hatukuwa na maandalizi mazuri ya msimu.

Kila timu itakuwa inaanza kuvuna kile ambacho ilikipanda kuanzia kwenye bechi la ufundi mpaka kwa wachezaji.

Kama kuna timu zilipata makocha wazuri, itakuwa ni wasaa wa kuonesha ufundi wa kile ambacho wanakifundisha na kama usajili ni mzuri, tutaona wachezaji wakikionesha uwanjani.

Najua hakuna ligi yoyote duniani ambayo timu zote zinashinda na kwenye msimamo ni lazima iwe timu inayoongoza na kati na nyingine inayoshika mkia, lakini tunachohitaji timu zipambane.

Hatuwezi kuwa na ligi nzuri ambapo tunaona mwanzo tu, baada ya michezo mitano mpaka sita, mashabiki wameshaanza kujua timu zinazowania ubingwa, nne bora na zile ambazo zitakuwa zinapigania kushuka daraja.

Inachosha kuona baada ya michezo kadhaa unaanza kuona kuna timu moja au mbili ambazo hazijiwezi kabisa, badala yake zinagawa pointi.

Nikitoka huko nakwenda kwa waamuzi. Wamekuwa wakilalamikiwa mara kwa mara kuhusu maamuzi yao ambayo yamekuwa yakiziathiri timu zingine.

Wakati mwingine mashabiki wanaweza kuiona timu fulani ni nyanya, lakini kumbe inaathiriwa zaidi na maamuzi ya marefa.

Waamuzi wakumbuke kuwa safari hii timu zimejipanga kweli kweli, zimesajili wachezaji wengi wazuri na zipo ambazo miaka mingi hazikuwa zinasajili wachezaji wa kigeni, safari hii zimefanya hivyo.

Lengo ni kupata wachezaji bor watakaoleta upinzani mkubwa kwenye ligi. Haiwezekani watu waingie gharama kubwa kiasi hicho halafu, mtu mmoja tu na filimbi yake katikati anainyonga na kufifisha juhudi na gharama ambazo viongozi wameingia.

Wakati mwingine waamuzi huwaponza makocha wanafukuzwa. Kosa la mwamuzi linaweza kusababisha viongozi kumwajibisha kocha wakati halikuwa la kiufundi, bali refa amesababisha. Tumeona sana hayo yakitokea kwenye Ligi Kuu.

Waamuzi wanapaswa wawe na huruma na makocha kwani nao ni ajira zao ambazo zinawapatia mkate wao wa kila siku na familia, lakini makosa yao ya makusudi au bahati mbaya yanazima ndoto za wenzao.

Ina maana dhambi ya makosa ya waamuzi, yanabebwa na makocha. Ndiyo maana nimefarijika kumsikia Raisi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Wallace Karia, hivi karibuni, akisema safari hii hawatomfungia mwamuzi atakayevurunda tu, bali wanaweza kumwondoa kabisa, akafanye shughuli zingine. Nadhani hii inaweza kuwa mwarobaini ili kila timu ishinde kwa kile ilichokipanda.