Tuangalie upya mizani ya elimu yetu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:59 AM Sep 09 2025
Wanafunzi
Picha: Mtandao
Wanafunzi

KILA kizazi hupimwa kwa namna kinavyowalea na kuandaa watoto wake. Naomba nilete mjadala muhimu kwa taifa letu kuhusu kazi za nyumbani (homework). Swali kuu la tafakuri ni hili: je, kazi hizi ni nyenzo ya kukuza elimu na maarifa, au ni mzigo unaowanyang’anya watoto muda wao wa familia, michezo, mapumziko na ndoto zao?

Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hatuwezi kukwepa mjadala huu. Huu si mjadala wa vitabu na kalamu pekee, bali ni mjadala wa utu, malezi na mustakabali wa taifa.

Mizani ya Utoto na Elimu

Watoto wetu hutumia saa saba hadi nane skuli kila siku. Baada ya masomo marefu na nidhamu za darasa, kengele ya mwisho inapolia, tunapaswa kujiuliza: je, watoto hawa wanapaswa kuendelea kubeba makaratasi ya kazi, au wanastahili kurudi nyumbani kupata nafasi ya kukua kijamii, kifamilia na kiubunifu?

Elimu si wingi wa maarifa pekee, bali ni hekima ya kuyatumia kwa ajili ya maisha. Utoto ni kipindi cha kipekee na kifupi sana ambapo michezo, sanaa, simulizi na mafunzo ya kifamilia huchonga utu na roho ya mtoto. Tukiwajaza watoto mzigo wa kazi zisizoisha, tunatengeneza kizazi cha wajuzi wa kukariri, lakini maskini wa fikra, maskini wa ubunifu na pengine maskini wa furaha.

Kwa mfano, ripoti ya UNICEF (2019) ilibaini kuwa watoto wanaopata muda zaidi wa kucheza na kushirikiana na familia hufanya vizuri zaidi katika ujuzi wa kijamii na kiakili kuliko wale wanaofungwa na masomo pekee. Aidha, tafiti nchini Finland zinaonesha kuwa licha ya wanafunzi wao kuwa na muda mdogo wa masomo darasani na kazi za nyumbani, taifa hilo linaendelea kushika nafasi za juu katika matokeo ya kimataifa ya elimu (PISA).

Mfano Kutoka Maisha ya Watu Wazima

Katika dunia ya ajira, hakuna mwajiri anayetarajia mfanyakazi wake kurudi nyumbani na kuendelea na masaa manne ya kazi bila malipo. Sheria za kazi na utu wa kibinadamu zinatambua haki ya kupumzika. Ikiwa watu wazima tunalindwa na haki hii, kwa nini tusiheshimu zaidi miili na akili za watoto wetu ambao bado wako katika hatua ya ukuaji?

Kwa hakika, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza kuwa watoto wanapaswa kupata angalau saa moja ya michezo ya mwili kila siku ili kuimarisha afya ya mwili na akili. Lakini mzigo mkubwa wa kazi za nyumbani mara nyingi huwapokonya nafasi hiyo.

Wito wa Kufafanua Upya Kazi za Nyumbani

Hoja yangu si kufuta kabisa kazi za nyumbani. Bali ni wito wa kuzifafanua upya. Kazi ziwe nyepesi, zenye maana na za nadra—miradi ya kuchochea udadisi, mijadala ya kifamilia au maandalizi ya somo lijalo.

Mtoto anayesaidia mzazi jikoni, anayesikiliza hekaya za babu na bibi, anayesoma kitabu kwa hiari au anayecheza mpira na kuogelea na marafiki, anajifunza masomo ya maisha ambayo karatasi haiwezi kufundisha. Hapo ndipo elimu inapogeuka kuwa uhai, si maneno matupu.

Takwimu za OECD (2018) zinaonesha kuwa wanafunzi wa Japan hutumia wastani wa saa moja tu kwa kazi za nyumbani ambazo ni za nadra—lakini bado taifa hilo ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza duniani kwa taaluma ya sayansi na hisabati. Hii ni ishara kwamba ubora wa elimu hauko katika wingi wa kazi za nyumbani, bali katika mbinu na mizani yake.

Utoto ni ua dogo linalochanua mara moja tu katika bustani ya maisha. Tukiliwekea mizigo isiyo na mizani, tutalivunja kabla halijakua. Lakini tukililinda kwa furaha, michezo na malezi bora, tutavuna taifa lenye hekima, ubunifu na mshikamanio.

Zanzibar na Tanzania tuna nafasi adhimu ya kuongoza wengine kwa dira hii mpya ya elimu:

“Kazi za nyumbani zibakie skuli; nyumbani kubakie ni chemchemu ya familia, furaha na ndoto.”

Khalēd Gwiji

+1 437 431 6747