SHULE zimefunguliwa baada ya kukamilika mapumziko mafupi ya muhula wa pili kuelekea kukamilisha mwaka wa masomo wa 2025
Ni wakati wa kampeni pia na kuahidi kazi zitakazofanywa ndani ya siku 100 za mwanzo ikulu, kwa hiyo tunakumbusha kuwa mojawapo ya vikwazo kwa shule za msingi, ni upungufu wa madawati, huku baadhi ya maeneo yakiwa na misitu ya kutosha.
Mbao zipo na zingepunguza changamoto hiyo kwenye shule nyingi. Hivyo wagombea hilo ni jukumu lenu. Hakuna cha kujitetea, mtangaze mnalimalizaje.
Kwa muda mrefu sasa vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikiripoti kuwapo kwa upungufu huo wa madawati unaosababisha baadhi ya wanafunzi kusomea katika mazingira yasiyo rafiki kwao.
Zipo shule nyingi za changamoto hiyo, mojawapo ikiwa ni Shule ya Msingi Kasisiwe iliyoko Mpanda mkoani Katavi inayokabiliwa na upungufu wa madawati 750.
Akisoma taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu, Jane Sigarate katika mkutano wa wazazi na maofisa elimu anasema ina jumla ya wanafunzi 3,000 na madawati 164 tu.
Kwa mujibu wa Mwalimu Jane kuna upungufu wa madawati 750 kwa msimu wa mwaka huu wa 2025, na anawaomba wazazi kujitokeza kuchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati.
Tatizo hilo kwa shule hiyo tu bali lipo katika maeneo mengine ya nchi na linasababisha baadhi ya wanafunzi kukaa katika mavumbi, kitendo kinachoweza kusababisha wasisome kwa ufanisi.
Ninadhani umefika wakati sasa kutafuta namna na kujitegemea badala ya kutegemea wafadhili hata kwenye suala la madawati, huku nchi ikiwa na misitu mingi ambayo ingetumika kutengeneza madawati.
Na hilo wagombea wanalazimika kulitatua haraka iwezekanavyo ikibidi ndani ya siku 100.
Ipo haja ya kuanzisha kampeni maalum za kuhakikisha kila shule inakuwa na madawati ya kutosha yanayotokana na misitu iliyopo ili kuwapunguzia wazazi na walezi mzigo wa kuchangia madawati kila mwaka.
Wao wanaweza kubaki na jukumu la kuchangia chakula shuleni ambacho nacho bado ni changamoto kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo baadhi yao kugoma kuchangia wakiamini kuwa ni jukumu la serikali.
Hivyo, ni vyema uongozi utakaoingia madarakani ushirikiane na kamati za shule kuchonga madawati ya kutosha yanayotokana na mbao za misitu mbalimbali badala ya kusubiri kupata ya msaada.
Kamati na bodi ndizo zenye kupanga mipango ya kuboresha shule kwa kushirikisha wananchi ili waweze kuzihudumia badala ya kujiweka pembeni na kudhani hawahusiki.
Sio kwamba ninapinga madawati ya msaada, bali ninahamasisha umuhimu wa kujitegemea kwa kutumia misitu, kwani ni aibu kuona shule ambayo ipo na msitu wa mbao haina madawati.
Lakini pamoja na changamoto ya upungufu wa madawati, upo pia mwingine wa wa matundu ya vyoo kwenye shule mbalimbali, kamati za shule ndizo zenye kupanga mipango ya kuboresha shule kwa kushirikisha wananchi ili waweze kuzihudumia.
Sidhani kwamba ni kosa wananchi kuchimba mashimo ya vyoo, kufyatua matofali na kujenga na kwa ajili ya watoto wao. Suala la msingi hapa, ni kuimarisha mfumo wa uwajibikaji na ushirikishaji wa wananchi kwa mambo ambayo yanawahusu, ili nao watimize wajibu.
Ninaamini ujenzi wa vyoo vya shule umo ndani ya uwezo wa umma si wa kutafuta au kusubiri wafadhili. Jambo la muhimu ni serikali iwekeze kwenye miundombinu hiyo na kamati kushirikisha wananchi au wazazi na walezi ili nao wawe na mchango.
Kamati za shule zikifanya sehemu yake ya kushirikisha na kuhamasisha wananchi, huku serikali mpya nayo ikisaidia katika juhudi za kumaliza matatizo yanayozikabili shule za umma.
Pamoja na hayo, ipo haja ya kutafuta vyanzo vya fedha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya shule ili hatimaye changamoto mbalimbali zinazokabili shule za msingi kubaki historia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED