Kampuni ya Acer Inc., moja ya vinara wa kimataifa katika suluhisho za kisasa za teknolojia, imetangaza rasmi upanuzi wake wa kimkakati katika soko la Afrika Mashariki, ikilenga kuchochea mabadiliko ya kidijitali kupitia bidhaa za kiwango cha juu kwa watumiaji wa aina mbalimbali.
Katika mpango huo mpya, Acer inaleta safu kamili ya bidhaa zenye uwezo wa hali ya juu, kutoka kwa vifaa vya kiwango cha mwanzo hadi vile vya kiwango cha juu kabisa. Bidhaa hizo zimebuniwa mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara, sekta ya elimu, watumiaji wa kawaida pamoja na wapenzi wa michezo ya mtandaoni (gamers), huku zikiakisi dhamira ya kampuni hiyo kusaidia maendeleo ya kidijitali barani Afrika kupitia teknolojia ya kuaminika, salama na bunifu.
“Lengo letu ni kuwezesha wafanyabiashara, shule na familia katika Afrika Mashariki kupitia teknolojia itakayoleta tija, ubunifu, burudani na uunganishwaji kiteknolojia,” alisema Grigory Nizovsky, Makamu wa Rais wa Acer kwa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika.
Aliongeza kuwa Acer imejikita katika kuondoa vizuizi vya mawasiliano baina ya watu kwa lengo la kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali zinazokumba jamii ya kisasa.
Acer imetambuliwa kimataifa kama mshirika thabiti katika sekta ya elimu kwa kutoa vifaa vinavyosaidia mazingira ya kujifunza kwa njia ya kidijitali. Kupitia bidhaa kama Chromebook, kompyuta mpakato na teknolojia za madarasani, kampuni hiyo inaendelea kusaidia taasisi za elimu kuendana na mahitaji ya karne ya 21.
Kwa mujibu wa taarifa yao, elimu ni eneo la kipaumbele kwa kampuni hiyo kwa kuwa ndicho chanzo kikuu cha maendeleo endelevu na ujumuishaji wa kidijitali, sambamba na kaulimbiu yao ya "Kuondoa vizingiti kupitia teknolojia."
Katika soko la Afrika Mashariki, bidhaa za Acer zimegawanywa katika makundi matatu makuu:
Kupitia safu ya Aspire Vero, Acer pia imeonyesha kujitolea kwake kwa mazingira. Vifaa hivi vimetengenezwa kwa kutumia plastiki iliyosindikwa na vinaweza kutengenezwa upya kwa urahisi. Safu hiyo ni sehemu ya mkakati wa Acer wa kuwa kampuni isiyo na utoaji wa hewa ukaa (carbon neutral) ifikapo mwaka 2050.
Kwa kutambua juhudi hizi, Acer imeorodheshwa kwenye Kielelezo cha Uendelevu cha Dow Jones (DJSI) cha Dunia 2024, na pia kutajwa na jarida la Forbes kama moja ya Kampuni Bora kwa Wanawake Duniani kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa bidhaa na kuboresha huduma kwa wateja wa Afrika Mashariki, Acer inaimarisha mnyororo wake wa usambazaji na kupanua maeneo ya uzalishaji. Hivi sasa, kampuni hiyo ina uwezo wa kuunganisha bidhaa katika nchi mbalimbali kama India, Brazil, Indonesia, Afrika Kusini, na Marekani, hatua inayoiwezesha kushiriki zabuni za serikali na kuhudumia wateja wa ndani kwa ufanisi zaidi.
Sriram Sundaram, Meneja Mkaazi kwa nchi zilizosalia Afrika, alieleza kuwa kampuni hiyo inatumia uzoefu wa mafanikio kutoka masoko mengine duniani kuunda suluhisho bunifu na rafiki kwa watumiaji wa Afrika Mashariki.
“Tutashirikiana na washirika wa ndani kutoa huduma baada ya mauzo, mafunzo, na hata fursa za msaada wa kifedha kwa wateja wetu,” alisema Sundaram.
Acer ilianzishwa mwaka 1976 na sasa ni miongoni mwa makampuni makubwa ya teknolojia duniani, yenye uwepo katika zaidi ya nchi 160. Ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 7,800 duniani, kampuni hii inaendelea kuwekeza katika uvumbuzi wa teknolojia, ukuaji wa kidijitali, na maendeleo endelevu kijamii na kimazingira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED