CAG: Milioni 892.92 zilililipwa bila vipimo vya kazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:55 AM Apr 22 2025
Fedha.
Picha: Mtandao
Fedha.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema amebaini kuwa miradi minne ililipa jumla ya Sh. 892.92 kwa mafundi na wakandarasi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu bila kutumia nyaraka za vipimo vinavyothibitisha kazi zilizotekelezwa.

Miundombinu hiyo ni ya shule na vyuo vya walimu, ikiwa pamoja na madarasa, matundu ya vyoo, majengo ya utawala, mabweni, na majiko.

“Kasoro hii ilikotokana na upungufu wa watumishi katika idara ya ujenzi kulikosababisha kuidhinishwa kwa malipo bila kuhakikiwa kwa kina, kutathmini, na kupima kazi zilizofanyika. Maelezo ya kazi ambazo zilifanywa bila nyaraka za vipimo,”amesema.


Katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24 kipengele cha usimamizi wa fedha, matumizi na bajeti, amesema idara ya ujenzi kuidhinisha malipo bila kukagua na kupima kazi iliyokamilishwa kunaongeza hatari ya malipo ya ziada, malipo ya kazi isiyokamilika, na uwezekano wa matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Ninapendekeza wasimamizi wa miradi wahakikishe kuwa kazi zinakaguliwa na kupimwa kabla ya kuidhinishwa,”amesema.


CAG amesema Kanuni ya 243(2) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 inazitaka taasisi zinazofanya ununuzi ziidhinishe malipo kwa kuzingatia vipimo vilivyoidhinishwa katika vipindi maalumu vya mkataba.

Aidha, Aya ya 25.3 ya Mwongozo wa Utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi kwa Utaratibu wa Nguvukazi (force account) uliotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wa Mei 2020 unaelekeza kuwa vipimo vya pamoja vya kazi zilizokamilika vifanywe na meneja wa mradi kwa kushirikiana na taasisi inayotekeleza mradi.