DC Kilakala atoa wito kudumishwa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 05:04 PM Jul 09 2025
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, ametoa wito kwa wananchi kuacha kushawishika na makundi yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, na badala yake wawe mstari wa mbele kuimarisha utulivu wa nchi, hasa katika kipindi hiki kinapokaribia uchaguzi mkuu.

Kilakala aliyasema hayo jana katika Tamasha la Amani la muziki wa Injili lililoandaliwa na The Healing Missionary kwa kushirikiana na Almee Sebene, lililofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani ya daladala, mkoani Morogoro.

Akizungumza katika tamasha hilo, Mjumbe wa Baraza la Amani Taifa, Happy Masawe, alihimiza umuhimu wa kuendeleza amani nchini kwa kuwa ikivunjika, wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi.

"Amani ikivunjika wanawake ndio hupata shida kubwa, hasa wakiwa na watoto. Ni muhimu wanawake wawe chimbuko la amani, waianze nyumbani mwao, na waendelee kuitafuta hata wanapokwenda katika familia nyingine," alisema.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Idara ya Vijana kutoka Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Jamali Jumaa, alitoa onyo kwa wananchi juu ya madhara ya kuchezea amani waliyonayo.

"Tusiichezee amani tuliyo nayo. Tujifunze kutoka kwa wenzetu katika mataifa kama Rwanda na Kongo, ambapo uvunjifu wa amani uliwapelekea kupoteza wapendwa wao na kuachwa na makaburi pekee," alisisitiza.

Naye Mkurugenzi wa Almee Sebene Morogoro, Meshack Shetente, alisema waliamua kuandaa tamasha hilo maalum Julai 7, kwa ajili ya kuiombea nchi amani kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Alisema wamechagiza nguvu ya maombi wakitumia andiko la Biblia kutoka Mathayo 7:7 linalosema “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona”, wakiamini kuwa amani ni jambo la msingi kwa ustawi wa taifa lolote, hasa katika nyakati za uchaguzi.

"Tunaamini kuwa amani ni kitu cha msingi sana, ndiyo maana tukatenga siku hii kuungana katika maombi ya kuiombea nchi yetu, tukitafuta uso wa Mungu ili Tanzania iendelee kuwa ya amani hata wakati wa uchaguzi mwezi Oktoba," aliongeza Shetente.