Dk. Mwinyi: Zanzibar ina nafasi kubwa kuongeza uzalishaji wa karafuu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:09 PM Oct 23 2025
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha; Mpigapicha Wetu
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji wa karafuu kutokana na kuwa na kiwango cha ubora wa juu duniani.

Ametoa kauli hiyo jana katika muendelezo wa utoaji wa hati miliki za mashamba ya mikarafuu kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba, ambapo alikabidhi hati 21 kwa wamiliki wa mashamba hayo.

Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatambua mchango mkubwa wa zao la karafuu katika kukuza uchumi wa nchi na kuinua maisha ya wakulima, na ndiyo maana imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazolikabili zao hilo.

Ameeleza kuwa licha ya ubora wa karafuu ya Zanzibar kutambulika kimataifa, kiwango cha uzalishaji bado ni kidogo, hali inayosababisha nchi kukosa tija kubwa kiuchumi.

“Uzalishaji wa karafuu kwa sasa hauzidi tani kumi kwa mwaka. Hii haitupi tija ya kutosha, wakati karafuu ya Zanzibar ndiyo bora zaidi duniani,” alisema Dk. Mwinyi.

Akitolea mfano, Dk. Mwinyi alisema Indonesia huzalisha zaidi ya tani 100,000 za karafuu kwa mwaka, akibainisha kuwa Zanzibar nayo ina uwezo wa kufikia uzalishaji mkubwa endapo changamoto zilizopo zitashughulikiwa ipasavyo.

Amesema Serikali imebaini changamoto kuu nne zinazochangia kushuka kwa uzalishaji wa karafuu, ikiwemo tatizo la umiliki wa mashamba. Alisema baadhi ya wakulima wamekuwa wakishindwa kuyahudumia mashamba yao kutokana na kukata tamaa, huku wengine wakikodisha mashamba hayo kwa watu wasiokuwa na dhamira ya kuyaendeleza, bali huvuna tu bila kuyatunza.