Gharama usajili pembejeo za kibailojia kikwazo kwa wabunifu

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:38 PM Apr 26 2025
Watafiti, wataalam wa kilimo, wakulima wa sekta ya Agrobiologicals nchini, wakiwa katika picha ya pamoja, baada ya kujadili mambo mbalimbali yanayoikabili sekta hiyo nchini.
Picha: Godfrey Mushi
Watafiti, wataalam wa kilimo, wakulima wa sekta ya Agrobiologicals nchini, wakiwa katika picha ya pamoja, baada ya kujadili mambo mbalimbali yanayoikabili sekta hiyo nchini.

Sekta ya pembejeo za kilimo cha kibailojia nchini (Agrobiologicals), inatishiwa na changamoto ya gharama kubwa za usajili wa pembejeo ambazo hazitumii kemikali, ambapo taratibu za kisheria zinaelekeza kulipwa Dola za Marekani 5000, sawa na Sh. milioni 13 za Tanzania.

Wakulima na wadau wa mnyororo wa thamani wa sekta hiyo, wamemuomba Rais, Samia Suluhu Hassan, kuzitazama changamoto zinazoikabili sekta hiyo hasa suala la usajili kwa jicho la tatu, ili kuwavutia wabunifu startups.

Baadhi ya wadau hao, akiwamo Meneja Mshauri wa Kiufundi (Technical Consultant Manager) wa Kampuni ya Koppert Biologicals Tanzania Ltd, Fredrick Tesha, amesema gharama kubwa zinaweza kufifisha jitihada za wabunifu wadogo au kuua mawazo ya wabunifu, ambao wanaanza au ni wa chini.


Alikuwa akizungumza Jijini Arusha jana, wakati wa warsha ya siku mbili ya watafiti, wakulima, wataalam wa kilimo na wazalishaji na wasambazaji wa pembejeo za kibaiolojia,

Watafiti, wataalam wa kilimo, wakulima wa sekta ya Agrobiologicals nchini, wakiwa katika picha ya pamoja, baada ya kujadili mambo mbalimbali yanayoikabili sekta hiyo nchini.

Warsha hiyo ya siku mbili iliyopewa jina la ‘2nd SIANI East African Agrobiologicals Experts Group Workshop’, iliandaliwa na Swedish International Agriculture Network Initiative, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Stockholm Environment Institute.

Akizungumzia kuhusu usajili, Mhadhiri na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Mesia Ilomo amesema,“Katika mazingira halisi ya wabunifu, Watanzania na hasa wale wadogo wadogo, hicho ni kikwazo. Kanuni zetu na sheria zinachukulia wabunifu wa uzalishaji wa Agrobiologicals kama wanafanana, ingawa kiuhalisia wako tofauti.


…Unaweza kuona mbunifu anayeanza kabisa kwenye hilo eneo, tunaita start-ups, ukimchukulia huyo na kampuni kubwa ambazo zina uwezo, wote wawe na hicho kiwango au mtaji usiopungua milioni 10 au zaidi kwenye usajili, tunakuwa tunaua pengine vipaji au mawazo ya wabunifu, ambao wanaanza au ni wa chini.”