Mfumo wa mnada kwa njia ya TEHAMA kupitia Tanzania Mercantile Exchange (TMX) umeendelea kuwa mkombozi kwa wakulima na wanunuzi wa korosho, kutokana na kuongeza uwazi, ushindani na ufanisi katika uendeshaji wa minada nchini.
Hayo yamebainishwa wakati wa uzinduzi wa mnada wa kwanza wa korosho kwa msimu wa 2025/2026 uliofanyika Kibiti, mkoani Pwani, ambapo mfumo huo ulielezwa kuwa chachu ya kuongeza thamani na bei ya zao hilo muhimu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa (TMX), Godfrey Malekano, alisema mfumo huo umeondoa changamoto nyingi zilizokuwepo kwenye minada ya jadi, kwani unaruhusu uwazi wa hali ya juu kwa pande zote—wauzaji na wanunuzi.
“Mfumo huu ni wa uwazi na haki. Wauzaji wanaona wazi namna wanunuzi wanavyoshindana kuomba bei. Mnunuzi anayetangaza bei ya juu ndiye anayeibuka mshindi wa mzigo,” alisema Malekano.
Ameongeza kuwa mfumo huo unamuwezesha mnunuzi kushiriki minada akiwa popote duniani, ikiwemo India au Vietnam, mradi tu ametimiza masharti, hivyo kupunguza gharama za safari na miamala.
Aidha, aliwataka wakulima wa korosho kuhakikisha wanatunza zao lao kwa kulikausha vizuri ili kuepuka unyevu, unaosababisha kupungua kwa ubora na bei sokoni.
Akizungumzia mabadiliko ya bei msimu huu, Malekano aliwahimiza wakulima kutokata tamaa, akisema bei hubadilika kadiri ya uhitaji wa masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, alisema serikali inaendelea kuhakikisha mkulima ananufaika moja kwa moja na zao la korosho kulingana na ubora wa mazao yao.
Amesema mfumo wa madaraja umeimarishwa zaidi, ambapo korosho daraja A na B ziko kwenye maeneo yake maalum kabla ya kuuzwa.
“Wakulima watalipwa kulingana na daraja la korosho zao. Hii itawajengea motisha ya kuboresha ubora,” alisema Alfred, akisisitiza umuhimu wa kukaushwa vizuri kwa korosho kabla ya kufikishwa sokoni.
Aliongeza kuwa zaidi ya tani 100,000 za korosho zimekusanywa hadi sasa, huku asilimia 13 ya korosho hizo zikiuzwa kwa bei ya chini, na serikali ikiendelea kufuatilia mwenendo wa bei hizo.
Naye Meneja wa CoRECU Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, alisema mnada huo wa kwanza umeonyesha mafanikio makubwa, ambapo tani 594 za daraja la kwanza na tani 616.931 za daraja la pili ziliingizwa sokoni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa:
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED