MNRT SACCOS yafanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 1.2 kwa mwaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:26 PM Oct 25 2025
MNRT SACCOS yafanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 1.2 kwa mwaka
Picha: Mpigapicha Wetu
MNRT SACCOS yafanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 1.2 kwa mwaka

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha MNRT SACCOS LTD kimefanikiwa kutoa mikopo kwa wanachama wake zaidi ya bilioni 1.2 kwa mwaka ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bernard Marcelline katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa tano (5) wa chama cha MNRT SACCOS LTD uliofanyika katika ukumbi wa TANAPA leo Oktoba 25,2025 jijini Dodoma.

Marcelline amesema kuwa chama hicho chenye wanachama zaidi ya 700 kimewezesha kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi kwa kufanya watumishi kuwa watulivu katika maeneo ya kazi kutokana na uhakika wa kipato.

“Kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 1.2 kwa mwaka maana yake ni fedha zimeingia kwa wanachama na zimekwenda kufanya shughuli za kiuchumi za maendeleo katika sehemu wanazoishi” amesema Marcelline.

“Nawahimiza watumishi wengine ambao hawajajiunga na saccos wajiunge na sacos hii kwa sababu inakua kwa haraka sana” amesisitiza Marcelline huku akiwahimiza waliokopa kutumia mikopo hiyo kwa malengo waliyojiwekea na pia kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwajengea uaminifu.

Naye, Mwenyekiti wa MNRT SACCOS LTD, Wilfred Msemo amesema kuwa Saccoss hiyo imefanikiwa kutoa gawio la shilingi milioni 76 kwa wanachama wake, kuchangia katika kuhudumia jamii yenye mahitaji mbalimbali pamoja na kuingiza wanachama wapya 138.