Prof. Assad: Uchumi wa Tanzania wapaa, ataka vijana wapewe ujuzi wa vitendo

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 04:36 PM Oct 22 2025
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Profesa Mussa Juma Assad.
Picha: Ashton Balaigwa
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Profesa Mussa Juma Assad.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), Profesa Mussa Juma Assad, amesema kuwa hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ni nzuri ukilinganisha na miaka ya nyuma, huku ukuaji wa uchumi ukiendelea kwa kasi na mfumuko wa bei ukiwa katika viwango vinavyoridhisha.

Akizungumza katika Kongamano la Kitaaluma la kujadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuishi kuelekea Dira 2050, lililoandaliwa na MUM kwa ushirikiano na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Profesa Assad amesema uchumi wa nchi umekua kwa wastani wa asilimia 6 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

“Kwa jumla uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia sita. GDP, kupanda na kushuka kwa pato la taifa kumekaa vizuri ukilinganisha na nchi jirani. Hali ya kiuchumi ni nzuri zaidi kuliko Kenya na Rwanda,” amesema Profesa Assad, ambaye pia ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu.

Profesa Assad amesema kuwa vigezo vya kiuchumi vya sasa vinaonyesha uwezo bora zaidi wa wananchi kuendesha maisha yao ukilinganisha na miaka ya nyuma, jambo linalodhihirisha uimara wa uchumi wa nchi.

Akizungumzia kuhusu uchumi jumuishi, Profesa Assad amesisitiza kuwa miaka 25 ijayo itahitaji dhamira kubwa ya kuhakikisha kila Mtanzania anaingizwa kwenye mfumo wa kiuchumi, bila kubaki nje ya mzunguko wa uzalishaji na maendeleo.

Aidha, ameeleza changamoto ya vijana wanaohitimu vyuo vikuu kukosa ujuzi wa vitendo, akibainisha kuwa tatizo siyo kutokuwa sehemu ya uchumi, bali kukosa stadi za kazi.

“Vijana tunaowatoa vyuoni wanapaswa kupewa mafunzo ya ujuzi wa vitendo baada ya kumaliza masomo. Serikali na sekta binafsi zishirikiane kutoa kozi fupi za miezi mitatu ili kuwasaidia vijana kuwa na kitu cha kufanya wanapohitimu,” amesisitiza.

Hata hivyo, Profesa Assad ameonyesha wasiwasi kuhusu ukusanyaji wa takwimu unaotumia mifumo ya kizamani, akitoa wito kwa taasisi za serikali kuboresha mifumo ya kidijitali kama inavyofanyika kwenye ukusanyaji wa mapato.

“Takwimu nyingi bado zinakusanywa kwa kutumia makaratasi. Ni muhimu sasa kuhamia kwenye mifumo ya kisasa ya kidigitali ili taarifa ziwe sahihi na zinazopatikana kwa haraka,” amesema.