Rais Samia: Tutajenga reli za kisasa za ndani ya miji Dodoma, Dar

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 06:17 PM Nov 14 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Picha:Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imepanga kujenga reli za kisasa za ndani ya miji (urban rail) katika majiji ya Dodoma na Dar es Salaam ili kurahisisha huduma za usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akihutubia katika ufunguzi rasmi wa Bunge la 13, akibainisha kuwa miji hiyo inakua kwa kasi na hivyo inahitaji mifumo bora ya usafiri wa umma.

“Tunajenga reli hizo ili kuboresha usafiri kwenye majiji yanayokua kwa kasi kubwa. Kwa mfano, Dar es Salaam tunatarajia kuwa na wakazi milioni kumi ifikapo mwaka 2030. Kusahihisha njia za usafiri ni kurahisisha shughuli za kiuchumi,” amesema Rais Samia.

Amesema ujenzi wa reli hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali kuboresha usafiri wa mijini, kupunguza msongamano wa magari na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.