Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewataka wafanyabiashara wa mkoa huo na mikoa jirani kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo ili kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Ametoa wito huo leo Novemba 13,2025 wakati wa Mkutano na uzinduzi wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mhita, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Biashara Mkoa wa Shinyanga,amesema mkoa huo,umejaliwa fursa nyingi za uwekezaji na biashara katika sekta mbalimbali,zikiwamo za kilimo,mifugo,madini na kwamba sekta hizo zinatakiwa kuendelea kushamiri ili ziweze kukuza uchumi uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
“Kutokana na fursa zilizopo,mkoa wa Shinyanga unahitaji ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na zao la Pamba kwa kujenga viwanda vya vifaa tiba, viwanda vya mifugo,vifungashio,ujenzi wa shule,hospitali, nyumba za kulala wageni na hoteli,uwepo wa fursa hizi unatoa nafasi kwa sekta binafsi kuendelea kuwekeza na kukuza biashara zao,”amesema Mhita.
Ameongeza kuwa katika Mkoa huo,pia wametenga eneo maalum la kiuchumi Buzwagi Special Economic Zone pamoja na maeneo mengi kwamba wafanyabiashara wanapaswa pia kuwekeza kwenye eneo hilo.
Aidha,amesema jukwa hilo la biashara ni muhimu sababu linaunganisha sekta na serikali katika kuzungumza lugha moja kwa kujadili jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kukuza sekta binafsi na kutatua changamoto zote sababu ni mhimili muhimu wa kukuza uchumi.
Amesema, katika uboreshaji wa mazingira ya biashara kwa sekta binafsi kwamba tayari serikali imeshaanza kutatua changamoto za sekta binafsi ikiwamo tozo za ushuru wa maeneo ya malazi na huduma “Hotel na Service Levy”kutoka tozo za asilimia 10 na kufika asilimia 2 kwa ushuru nyumba kulala wageni na asilimia 0.3 kwenda asilimia 0.25 kwa ushuru wa huduma.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Shinyanga Jonathan Manyama,amesema sekta binafsi inatendelea kuwa karibu na serikali, huku akiipongeza kwa kuendelea kuweka jitihada za utatuzi wa changamoto mbalimbali ambazo zinaikabiri sekta hiyo.
Amesema,sekta hiyo ikiboreshewa mazingira vizuri ya biashara, Tanzania itakuwa na uchumi imara pamoja na kuongeza pato la taifa na la mwananchi moja moja.
Kauli Mbiu ya Mkutano na Uzinduzi wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Shinyanga inasema”Usimamizi Mzuri wa Mabaraza ya Biashara katika kuchochea ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa mazingira ya biashara katika Mkoa.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED