Serikali kuandaa mkutano wa wadau wa mazao ya mboga na matunda

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 12:19 PM Nov 07 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli.
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli.

Serikali imeandaa mkutano mkubwa wa wadau wa mazao ya mboga na matunda utakaowahusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kujadili maendeleo na changamoto za sekta hiyo muhimu ya kilimo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amesema mkutano huo utakuwa wa kila mwaka na utafanyika katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha sekta ya kilimo cha mboga na matunda.

Mweli amesema mkutano huo wa siku mbili utaleta pamoja wadau wa serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya maendeleo, ili kujadiliana kuhusu njia bora za kuinua kilimo cha mboga na matunda nchini.

“Mkutano huu utakuwa mkubwa sana na ni fursa ya kujadili changamoto na mafanikio ya sekta hii ambayo imekuwa kichocheo cha kuinua kipato cha wakulima wengi nchini,” amesema Mweli.

Aidha, amesema sekta ya mazao ya mboga na matunda ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa taifa na ustawi wa wananchi, hivyo kupitia mkutano huo wadau watapata nafasi ya kujifunza na kubaini fursa zilizopo katika kilimo hicho.

Ameongeza kuwa ukuaji wa sekta hiyo unaendelea kwa kasi, jambo linalohitaji miundombinu madhubuti ya usafirishaji na masoko, ili kuhakikisha mazao ya wakulima yanapata soko ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha kilimo, Mweli amesema tayari serikali imeanza kusambaza pembejeo kwa wakulima wote nchini, ili kuongeza tija na ubora wa mazao yanayozalishwa.