Serikali imetoa jumla ya tani 192 za mbegu bora za mazao mchanganyiko zenye thamani ya Sh bilioni 1.82, kwa ajili ya msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wakulima kulima kilimo chenye tija na kuongeza mavuno.
Mbegu hizo zimetolewa kupitia ruzuku ya serikali na zinalenga kufikia wakulima waliosajiliwa kwenye mfumo wa ruzuku na waliouza mazao yao kupitia masoko ya kidigitali.
Akizindua mpango wa Taifa wa ugawaji wa mbegu bora kwa wakulima jana mkoani Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alisema kati ya tani hizo 192, ufuta unachukua tani 126, mbaazi tani 16, choroko tani 17, dengu tani 30 na soya tani 3.
“Wakulima watakaonufaika na mbegu hizi ni wale waliojisajili kwenye mfumo wa ruzuku. Ugawaji utafanyika kupitia masoko ya kidigitali katika kila halmashauri, kuhakikisha kila mkulima anapata kwa uwazi na usawa,” alisema Mhita.
Aidha, Mhita aliwataka wakulima kuacha kuuza mazao yao kupitia mifumo isiyorasmi, akisema njia hizo zimekuwa zikiwanyima kipato stahiki na kuikosesha serikali mapato kutokana na kukosa takwimu sahihi za mauzo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, alisema mamlaka hiyo imetoa tani 3 za mbegu za choroko, sambamba na kutoa elimu ya kilimo chenye tija kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na kipato chao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Asangye Bangu, alisema wamefarijika kuona wakulima na wafanyabiashara wananufaika kupitia mfumo wa mauzo ya mazao kwa njia ya stakabadhi za ghala.
Mkulima Daison Cherehani kutoka Kijiji cha Shilabela wilayani Shinyanga alisema mfumo wa stakabadhi za ghala umewasaidia wakulima kuondokana na unyonyaji wa walanguzi.
“Kupitia mfumo huu, tumekuwa tukiuza kilo moja ya mazao kwa Sh 1,000 badala ya Sh 800 tulizokuwa tukipata kwa walanguzi. Hii imetusaidia kuinuka kiuchumi,” alisema Cherehani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED