Serikali imeahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima wa nafaka na mazao mchanganyiko ili kukuza uchumi wao, soko la ndani na nje na kuongeza pato la taifa kwa kukusanya ushuru.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao na Viwango wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Kamwesige Mtembei katika mkutano wa wadau wa zao la ufuta uliofanyika mkoani Songwe.
Mtembei, alisema serikali itaendelea kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora, kuhifadhi mazao kitaalamu na kuwa na soko la uhakika la ndani na nje ya nchi na kutoa ajira zaidi vijana wakiwemo maofisa ugani.
"COPRA tunashirikiana na wakulima kuanzia hatua za awali za uzalishaji mazao shambani hadi kwenye uuzaji kupitia mifumo ya stakabadhi ghalani na minada ya kidigitali," alisema Mtembei.
Akizungumzia zaidi kuhusu mifumo ya stakabadhi ghalani na minada ya kidijitali, alisema imeendelea kuleta tija na matokeo mazuri kwa wakulima wa zao hilo na mengine mkoani Songwe.
Alisema kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao hicho, kwa msimu uliopita pekee, wakulima pekee wa ufuta walipata zaidi ya Shilingi bilioni 42 kupitia mfumo huo.
Alisema hatua hiyo ilitoa msukumo taasisi moja kubwa ya fedha nchini kuhamasika kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.4 kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kwa wakulima ufuta 41 wa Wilaya ya Songwe na Momba.
Alisisitiza kuwa hiyo ni hatua kubwa kwa wakulima na kuongeza kuwa huo ni mwanzo na kwamba wataendelea kutoa ushirikiano kwao ili zao hilo limeendelea kuwaongezea zaidi mapato kwao na taif kwa kukusanya ushuru.
Mbali na taasisi hiyo, alisema nyingine yenye mtandao mkubwa nchini, ilitoa mikopo yenye thamani ya milioni 100 kwa AMCOS 10 za mkoani humo na kuahidi kutoa mingine maradufu ya pembejeo, zana mitaji kwa msimu ujao wa kilimo cha ufuta kwa wakulima mkoani humo.
Mmoja wa wakulima hao, Aneth William, aliishukuru serikali kwa kuwajali kwa kuwapa mikopo kwa ajili ya kuinua kilimo.
Aneth, aliwataka wakulima kuendelea kutumia fursa zinazotolewa na serikali kwenye sekta ta kilimo kujiajiri na kuajiri wengine na kuleta mapinduzi katika soko la ajira nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED