Utendaji kazi Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli, wamkosha 'kigogo' TUGHE

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:06 PM Oct 28 2025
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Taifa, Amani Msuya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Taifa, Amani Msuya.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Taifa, Amani Msuya ameeleza kuvutiwa na kiwango cha utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli kwa mwaka 2024/25 kufuatia Mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa zaidi ya asilimia 94.

Msuya ameeleza hayo  mkoani Morogoro wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika kwa lengo la kujadili, pamoja na mambo mengine, taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake  kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Nimevutiwa sana kusikia  mrejesho wa tathmini ya utekekelezaji wa mjukumu iliyofanywa kupitia Mfumo wa Tathmini ya Utendaji kazi, Mamlaka yenu ilitekeleza majukumu yake kwa asilimia 94.46 kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Kwa kiwango hiki cha utendaji kazi, ni dhahiri kuwa mnatekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa hakika ni jambo linalostahili pongezi” amesema Msuya. 

Msuya pia ametumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa Mamlaka hiyo, kutobweteka na kiwango cha tathmini cha mwaka wa fedha uliopita na badala yake waendelee kufanya kazi kwa juhudi zaidi ili kuongeza kiwango kwa mwaka 2025/26.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Charles Sangweni, amesema wataendelea kutekeleza majukumu yake kwa juhudi zaidi, weledi na ubunifu kwa kuzingatia mipango ya Taasisi.

Sangweni pia ametoa rai kwa watumishi wa Mamlaka hiyo, kuendelea kuzingatia ujazaji wa taarifa za utendaji kazi, kwa kuwa taarifa hizo ni moja ya nyenzo muhimu zinazotumika katika masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo kupandishwa vyeo.