Umoja wa Vijana wa Sekta ya Madini Tanzania (TYM) umewahimiza vijana kote nchini kuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani na kujiepusha na vishawishi vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TYM Taifa, Ashraph Omary, ambaye amesema kwamba mataifa yote yaliyoendelea hutegemea vijana kama nguvu kazi kuu ya taifa. Amesisitiza kwamba ni jukumu la vijana kujikita katika uzalishaji mali na kuachana na fikra au vitendo vinavyoweza kusababisha machafuko.
“Sekta ya madini inategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa amani na nguvu kazi ya vijana. Bila amani, ukuaji wa sekta hii muhimu unadumaa,” amesema Omary.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja huo, Cathberth Joseph, amesema TYM imeongezeka kutoka wanachama 600,000 hadi zaidi ya vijana milioni 4.6 nchini. Umoja huo unahusisha wadau wote katika mnyororo wa thamani wa madini, wakiwemo wachimbaji, mamalishe, wauzaji wa vifaa vya uchimbaji na wadau wengine wa sekta hiyo.
Joseph amebainisha kuwa vijana ni mtaji mkubwa wa maendeleo ya sekta ya madini, akitaja mfano wa zaidi ya vijana 2,000 waliopatiwa leseni za uchimbaji katika mgodi wa Nyamongo, mkoani Mara, hatua iliyowawezesha kiuchumi na kuchangia pato la taifa.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali vijana wachimbaji kupitia utoaji wa leseni 11 za uchimbaji na mitambo miwili ya kuchorongea dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 36.
“Nampongeza sana Rais Samia kwa kusaidia vijana kupata leseni na kupunguza gharama za kuchorongea dhahabu, ambazo sasa zimefikia shilingi 200,000 kwa mita moja. Hii ni hatua kubwa ya kuwawezesha vijana katika sekta ya madini,” amesema Joseph.
Katibu Mkuu Ashraph Omary amewataka vijana wachimbaji na wote waliopo katika sekta ya madini kuepuka kuandamana au kushiriki vurugu wakati wa uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kutumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura kwa amani, uhuru na haki.
“Amani ni msingi wa maendeleo. Vijana tuwe chachu ya umoja na siyo chanzo cha machafuko,” amesisitiza Omary.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED