Wafanyabiashara wa mafuta kuchukuliwa hatua

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 12:44 PM Apr 23 2025
news
Picha: Mtandao
Mafuta.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amesema mamlaka hiyo iko tayari kuchukua hatua kali dhidi ya baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta wanaoagiza mafuta kwa madai ya kuyapeleka nje ya nchi lakini badala yake wanayauza ndani, hali inayochangia kuvuruga soko la mafuta nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao na waagizaji na wasambazaji wa mafuta, Kamishna Mwenda alisema kuwa pamoja na wafanyabiashara hao kudai kuwa na vibali kutoka mamlaka mbalimbali, TRA itasimamia sheria na kuhakikisha kodi inakusanywa kwa usawa bila upendeleo.

“Moja ya malalamiko ya msingi kutoka kwa wafanyabiashara ni kutaka usawa kwenye ulipaji kodi. Haiwezekani wengine walipwe kodi na wengine wasamehewe. TRA tutachukua hatua kwa wale wanaovuruga ushindani wa soko kwa njia zisizo halali,” alisema.

Kamishna huyo aliongeza kuwa wafanyabiashara wanaojihusisha na aina hiyo ya udanganyifu si wengi na tayari wanajulikana. Alifafanua kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa TRA, mafuta yote yanayoagizwa kwa ajili ya kusafirishwa nje yanaruhusiwa kukaa nchini kwa muda wa siku 30. Iwapo muda huo utapita, kampuni husika inatakiwa kulipia kodi.

“Kuna kampuni ambazo hazina muda wa ziada, tumezishinikiza zilipie kodi kwa mujibu wa sheria. Tunataka kampuni zote zifuate taratibu bila kujali wamepata vibali kutoka kwa nani,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Mwenda, sekta ya mafuta ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, ikichangia takribani Shilingi bilioni 400 kwa mwezi kupitia kodi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta (TAOMAC), Raphael Mgaya, alisema kuwa kwa sasa soko la mafuta linakumbwa na changamoto ya bei kinzani, ambapo baadhi ya kampuni zinauza mafuta kwa bei ya chini hadi Shilingi 400 ukilinganisha na bei elekezi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

“Kwa hali hii, inaonesha kuna mafuta yanayoingizwa nje ya mfumo rasmi wa DPS na ndiyo yanayouzwa kwa bei ya chini na kuathiri ushindani wa haki. Tunaomba TRA itusaidie kudhibiti hali hii,” alisema Mgaya.

Aidha, aliiomba TRA iangalie uwezekano wa kupunguza presha ya ulipaji wa kodi kabla ya bidhaa kushuka bandarini, kwa kuwaruhusu wafanyabiashara kulipa asilimia 50 ya kodi wakati mzigo unaposhushwa, na kiasi kilichobaki kulipwa baada ya mwezi mmoja mzigo utakapokuwa umeshauzwa.

“Tangu mwaka 2020 biashara yetu imepata changamoto nyingi — kuanzia janga la corona, vita ya Urusi na Ukraine hadi upungufu wa dola. Wanachama wetu wengi bado wanahangaika kurejea katika hali ya kawaida,” alieleza.