Menejimenti ya Wizara ya Viwanda na Biashara imehimizwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi wanaohitaji huduma kutoka serikalini, ili kuimarisha misingi ya utoaji wa huduma bora na zenye tija kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hashil Abdallah, wakati menejimenti ikipata mafunzo kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), yanayofanyika mkoani Dodoma.
Dk. Abdallah amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubunifu kwa watumishi wa wizara katika kutekeleza majukumu yao ya kiserikali.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo yanahusu taratibu za usajili wa kampuni, majina ya biashara na alama za biashara na huduma, utoaji wa leseni za biashara na viwanda, matumizi ya mifumo ya kidijitali ya BRELA pamoja na huduma za ulinzi wa haki miliki za ubunifu.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha watumishi wa wizara wanapata uelewa wa kina kuhusu majukumu ya BRELA, taratibu za usajili, utoaji wa leseni na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ili wawe mabalozi bora wa kutoa ushauri wa kitaalamu na wa haraka kwa wananchi na wawekezaji.
Nyaisa ameongeza kuwa BRELA ni taasisi muhimu katika kukuza mazingira bora ya biashara nchini na kusimamia utekelezaji wa sheria sita za msingi, ikiwemo Sheria ya Makampuni, Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara, Sheria ya Gharama za Biashara na Huduma, Sheria ya Hataza, Sheria ya Usajili na Leseni za Viwanda, na Sheria ya Leseni za Biashara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED