Wakulima pareto wazitilia shaka maabara za wanunuzi

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 10:12 AM Jun 28 2024
Pareto.
Picha: Mtandao
Pareto.

WAKULIMA wa pareto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wameiomba serikali kuwasaidia kuweka utaratibu mzuri wa uendeshaji wa maabara za wanunuzi wa zao hilo, wakidai kuwa kuna mchezo mchafu unafanywa na wanunuzi.

Wakulima wa zao hilo katika kata za Santilya na Itawa waliwasilisha ombi hilo juzi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Beno Malisa alipofanya ziara ya kusikiliza kero za wakulima, ambapo walisema maabara hizo zinafanya kazi kwa kificho.

Mmoja wa wakulima hao, Cosmas Sishamba alisema wanunuzi wa pareto wanachukua sampuli na kwenda kupima kiwango cha sumu bila kuwa na uwakilishi wa wakulima na kuwaletea majibu kuhusu kile kilichobainika na kupanga bei.

Alisema hali hiyo inawapa wasiwasi kwamba huenda kile kinachobainika kwenye pareto hiyo ni tofauti na uhalisia na hivyo wanunuzi wakawa wanazitumia kuwapunja wakulima.

Aliomba serikali kuwaweka wataalamu wake kwenye maabara hizo ili wao ndiyo wasimamie badala ya kuwaachia wanunuzi kumiliki maabara na kupanga bei wao wenyewe.

“Mnunuzi anamiliki yeye mwenyewe maabara, anakwenda kupima kiwango cha sumu na kututajia bei kulingana na alichokiona kwenye pareto bila sisi wakulima ama serikali kushiriki, sasa tutapataje haki? Tunaomba serikali iwatumie wataalamu ambao imewasomesha ndiyo wasimamie maabara hizi,” alisema Sishamba.

Naye Philemon Wilias alisema miaka ya nyuma wakulima walikuwa wanashirikishwa kwenye vikao mbalimbali vya wadau wa zao hilo vikiwamo vinavyotumika kupanga bei lakini kwa sasa hawashirikishwi na badala yake wanalazimika kuuza kwa bei waliyopangiwa.

Alisema kwa sasa baadhi ya watu wanaoshiriki kwenye vikao na mikutano ya wadau wa pareto hawana ujuzi wowote na wala hawajui chochote kuhusu uzalishaji wa zao hilo na hivyo akaomba utaratibu wa kuwashirikisha wakulima urejeshwe.

Mkuu wa Idara ya Kilimo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Gideon Mapunda, alisema miaka ya nyuma kampuni za kununua pareto zilikuwa mbili pekee hali ambayo ilikuwa inasababisha ushindani wa bei kuwa mdogo.

Alisema wakati huo kilo moja ya pareto ilikuwa inanunuliwa kwa Sh. 2,000 lakini kwa sasa kampuni zilizosajiliwa zimefika sita na ushindani wa bei umeongezeka hali iliyosababisha bei kupanda mpaka Sh. 3,500 kwa kilo moja.

Hivyo, aliwataka wakulima kuendelea kufuata taratibu mbalimbali za uzalishaji wa zao hilo wanazofundishwa na wataalamu ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kukuza uchumi wao.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Malisa alisema serikali imeshaanzisha utaratibu wa kudhibiti uendeshaji wa maabara za kupima sumu ya pareto kwa kuanzisha siku maalumu ya kupima badala ya kila mnunuzi kupima kwa muda wake. 

Vilevile alisema kwenye kila maabara kuna maofisa wa serikali ambao wanafanya kazi ya kuhakiki upimaji wa sumu hiyo ili kuzuia wanunuzi hao kuwapunja wakulima kwa kutoa matokeo tofauti na uhalisia.