Zaidi ya vikundi 3,000 vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vimesajiliwa na serikali mkoani Mbeya ndani ya mwaka mmoja, huku vikundi 736 vikinufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ameyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu, wakati wa kongamano la wanawake na wafanyabiashara wadogo wa mkoa huo, lililokuwa na lengo la kutoa elimu ya kutambua na kuchangamkia fursa za kibiashara.
Haniu amesema vikundi hivyo vilisajiliwa ndani ya mwaka wa fedha 2024/2025 na baadhi ya vikundi vimejiunga kwenye majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayopatikana kwenye ngazi mbalimbali.
“Serikali imeendelea kuimarisha majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mkoa. Hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, jumla ya majukwaa 544 yapo ngazi ya vijiji, majukwaa 149 ngazi ya kata, majukwa 5 ngazi ya wilaya na jukwaa 1 ngazi ya mkoa,” amesema Haniu.
Haniu pia aliwahimiza wanachama wa vikundi vilivyokopeshwa mikopo ya asilimia 10 kurejesha kwa wakati ili vikundi vingine pia vinufaike na fursa hiyo. Vilevile aliwataka vikundi kuendelea kujiunga na majukwaa mbalimbali ili kunufaika na fursa nyingine za kibiashara na mikopo inayotolewa na serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED