Balozi Batilda aitaka Tanga kuchangamkia fursa za kilimo kwenye wiki ya chakula duniani

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 01:50 PM Oct 12 2025
 Balozi Batilda aitaka Tanga kuchangamkia fursa za kilimo kwenye wiki ya chakula duniani
PICHA: MTANDAO
Balozi Batilda aitaka Tanga kuchangamkia fursa za kilimo kwenye wiki ya chakula duniani

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian amefungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Chakula Duniani yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara mkoani Tanga tarehe 11-16 Oktoba 2025.

Akizungumza katika ufunguzi huo Balozi Dk. Burian amesema kuwa maadhimisho yanatoa fursa muhimu kwa wananchi na wadau wa Sekta ya Kilimo kubadilishana uzoefu, kuonesha ubunifu, na kujifunza teknolojia bora za kilimo chenye tija, ili kuimarisha uzalishaji wa chakula bora na salama nchini. Amesema Mkoa wa Tanga umejipanga kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakuwa chanzo kikuu cha ajira, kipato na maendeleo endelevu ya wananchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi ameeleza kuwa Sekta ya Kilimo nchini ipo katika kipindi cha mageuzi makubwa tangu mwaka wa fedha 2021/2022, hatua iliyolenga kuongeza tija, kuboresha uzalishaji na kuimarisha kilimo cha kibiashara. 

Dkt. Nindi amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku za mbolea, mbegu bora na viuatilifu; hatua ambayo imeongeza uzalishaji na kuiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa chakula sambamba na kuuza mazao katika masoko ya nje ya nchi.

Dkt. Nindi amesema kuwa ifikapo mwaka 2030, Sekta ya Kilimo inatarajiwa kukua kwa asilimia 10, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika utafiti, ubunifu na upatikanaji wa pembejeo bora ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata chakula chenye ubora na lishe. Aidha, alisisitiza umuhimu wa wadau wote kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza mipango ya kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya kilimo nchini.

Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wawakilishi wa Makatibu Wakuu, Viongozi wa dini, pamoja na Wadau wa Maendeleo na Taasisi za Sekta Binafsi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Tuungane Pamoja Kupata Chakula Bora kwa Maisha Bora ya Baadae”.