Tume Huru ya Uchaguzi yafuta kata 10 na kutengua wagombea saba wa Udiwani

By Rehema Matowo , Nipashe
Published at 12:09 PM Oct 12 2025
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza mabadiliko kwenye maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikifuta kata 10 na kutengua uteuzi wa wagombea saba wa udiwani waliokuwa wamekwisha teuliwa.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kufuta kata hizo kisheria kufuatia mabadiliko ya mipaka ya kiutawala na kutangaza baadhi ya maeneo kuwa makazi tengefu ya wakimbizi, kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 596 na 600 la Oktoba 3, 2025.

Kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Mishamo, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Milambo, Igombemkulu na Kanindo zikiwa katika halmashauri za Nsimbo, Tanganyika mkoani Katavi na Kaliua mkoani Tabora .

Uamuzi huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, Oktoba 12, 2025, kufuatia kikao cha Tume kilichofanyika Oktoba 6, 2025, na kuchapishwa katika Tangazo la Serikali Na. 604 la Oktoba 10, 2025.

Jaji Mwambegele, amesema kutokana na kufutwa kwa kata hizo, uchaguzi wa udiwani hauwezi kufanyika kwenye maeneo hayo, na hivyo wagombea waliokuwa wamekwishateuliwa hawatahusika tena kwenye orodha ya wagombea wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Aidha, Tume imefuta vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa na kuanzisha vituo vingine 292 katika kata jirani ili kuwahudumia wapiga kura 106,288 waliokuwa wamejiandikisha katika vituo vilivyofutwa.