Zitto: Nitapambana na ufisadi, kusimamia haki

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 05:18 PM Oct 12 2025
 
Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameahidi kupambana na ufisadi, kusimamia haki, na kuhakikisha Kigoma inakuwa kituo imara cha uchumi kama ilivyokusudiwa.

Zitto alitoa ahadi hizo leo, Oktoba 12, wakati akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Kigoma, akisisitiza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi kwa vitendo.

Amesema atachochea juhudi za kuifanya Kigoma kuwa Kituo cha Biashara na Uchukuzi wa Maziwa Makuu kwa kuimarisha Bandari ya Kigoma, kuhakikisha inaongeza thamani ya mizigo kutoka nchi jirani, na kwamba mikataba yote ya uendeshaji wa bandari inaleta manufaa kwa wananchi wa Kigoma.

Zitto ameahidi pia kusimamia kukamilika kwa mradi wa Chelezo cha Ujenzi wa Meli (Shipyard) Katabe–Bangwe, utakaotoa ajira na kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi wa ndani. Amesema atahakikisha reli ya SGR inafika Kigoma kwa wakati na kwamba eneo la stesheni litachaguliwa kwa manufaa ya jamii.

Akizungumzia historia ya uongozi wake wa awali (2015–2020), Zitto alikumbusha mafanikio yaliyopatikana wakati wa uongozi wa ACT Wazalendo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, akitaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa.

Alisema kuwa waliweza kujenga barabara za lami, kuanzisha masoko kama Soko la Jioni la Mzee Menge (Marungu), kuboresha Stendi ya Gungu, kujenga mialo ya wavuvi Kibirizi na kuanza ujenzi wa mwalo wa Katonga. Pia walijenga shule mpya, vituo vya afya, bandari mbili — Ujiji na Kibirizi — na kusukuma ujenzi wa Bandari Kavu ya Katosho.

Aidha, ameahidi kushughulikia kukamilika kwa Soko la Kimataifa la Mwanga na kuimarisha masoko ya jioni ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo. Pia ataharakisha ujenzi wa Soko la Kibirizi, ambalo litakuwa eneo lenye uhai kwa wafanyabiashara wa ndani.

Katika mipango yake, Zitto amepanga kufufua mji wa Ujiji na kurejesha hadhi yake kama kitovu cha biashara kupitia mradi wa Ujiji City, kushughulikia mafuriko katika Forodha ya Ujiji kwa kutumia teknolojia ya fabricated iron bars, na kuhakikisha boti za abiria zinaweka nanga katika Bandari ya Ujiji.

Pia ameahidi kujenga barabara ya Msimba–Ujiji, kuifanya Stendi ya Ujiji kuhudumia wasafiri wa ndani ya mkoa, kukamilisha Mradi wa Umwagiliaji Bonde la Luiche, kujenga daraja juu ya Mto Luiche, na kufungua Soko Kuu la Vyakula Ujiji.

Amesema ataanzisha mpango mkubwa wa kusafisha mitaa, kujenga mifereji ya maji ya mvua, na kugeuza maeneo kama mabwawa ya Katubuka kuwa fursa za kiuchumi ili kudhibiti mafuriko na kulinda mali za wananchi.

Vilevile, ataendeleza mipango ya miji ya pembeni kama Bangwe, Kagera na Gungu, kwa kupanga na kujenga miundombinu muhimu itakayorahisisha upatikanaji wa huduma.

Ameeleza kuwa atawawezesha vijana wa bodaboda kumiliki vyombo vyao kupitia mfuko maalumu wa mikopo, kurejesha mpango wa bima ya afya ya jamii, na kuondoa gharama za kujifungua kwa akina mama.

Zitto ameongeza kuwa atapigania kuanzishwa kwa Shule ya Ufundi na Chuo Kikuu cha Kigoma, ili kuwaandaa vijana kwa ujuzi wa kisasa na fursa za ajira.

Amesema atabaki kuwa sauti ya watanzania katika kupigania haki za uraia, ikiwemo upatikanaji wa NIDA, na kwamba hakuna atakayeachwa nyuma.

Akihitimisha hotuba yake, Zitto aliwataka wananchi wa Kigoma Mjini kutumia uchaguzi wa mwaka 2025 kama fursa ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa kuchagua ACT Wazalendo.