Jesca Magufuli: Samia ni mtu wa kazi apewe kazi, akafanye kazi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:32 AM Oct 12 2025
Jesca Magufuli
PICHA: CCM
Jesca Magufuli

Mgombea Viti Maalum kupitia kundi la vijana Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jesca Magufuli, ambaye ni mtoto wa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, amemnadi mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi Geita akisema, ni mtu wa kazi apewe kazi, akafanye kazi.

Akizungumza leo katika mkutano uliofanyika wilayani Bukombe, mkoani Geita, Jesca amesema wana kila sababu ya kumwamini na kutembea kifua mbele.
“Samia ni mtu wa kazi mpeni kazi akafanye kazi,” amesema.
Jesca amesema wana kila sababu ya kumwamini Samia  na kutembea kifua mbele na kuwaomba wananchi ikifikapo Oktoba 29, 2025, wakapige kura za ndio kwa mgombea wao wa urais, wabunge na udiwani wa CCM.
Akitoa salamu za Janet Magufuli, Jesca amweleza kuwa anamtakia kila la kheri katika safari hiyo ya urais, na kumwahidi  atakuwa mstari mbele kumwombea kura.
“Nimesimama kukuombea kura. Ndugu zangu mwenye macho haambiwi tazama, yote aliyofanya tumeona na kushuhudia, kwanza ni mchapakazi, jasiri, lakini mwenye maono mapana na makubwa,” amesema. 
Jesca alisema Samia alichukua kiti kipindi ambacho Rais Magufuli alifariki dunia, amefanya na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake na ameanzisha mwingine mipya.