JESHI la Polisi mkoani Arusha, limetaja sababu iliyosababisha mauaji ya askari wake, Omary Mnandi (30), kuwa chanzo chake ni ugomvi uliotokana na ajali ndogo inayodaiwa kusababishwa na gari lake.
Mnandi, aliyekuwa askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, anadaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana na kisha kupoteza maisha jana. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Mwandamizi Msaidizi (SACP), Justine Masejo, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 12 mwaka huu katika Baa ya Simaloi iliyopo eneo la Kaloleni, Jijini hapa.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo, ni ugomvi uliotokana na ajali ndogo ya magari, baada ya gari la marehemu lenye namba T.402 CNC kugonga gari jingine lenye namba T.734 AXR linalomilikiwa na mmoja wa watuhumiwa, jambo lililosababisha kutoelewana na kisha kushambuliwa.
Kwa mujibu wa Masejo, mpaka sasa jeshi hilo limewakamata na linawashikilia watuhumiwa watano kutokana na mauaji hayo.
Inaelezwa kuwa, kabla ya tukio hilo watuhumiwa hao wanadaiwa kumshambulia Mnandi na kumsababishia majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake, hali iliyosababisha kifo chake wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Kamanda Masejo, amesema Jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, na kwamba watuhumiwa watafikishwa mahakamani upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED