Wasafirishaji wa abiria kwa kutumia pikipiki (bodaboda) katika stendi ya Mlowo, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, wametakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali na kulinda usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
Elimu hiyo imetolewa Agosti 14, 2025 na Koplo Maganga Kalulumya kutoka Ofisi ya Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, alipokutana na madereva hao.
Koplo Maganga aliwakumbusha umuhimu wa kutumia vifaa vya kujikinga, ikiwemo helemu (kofia ngumu) inayolinda kichwa na koti lenye viakisi mwanga (reflectors) ili kuonekana kwa urahisi na magari mengine, hasa nyakati za usiku.
“Kuvaa helemu na koti la reflector siyo fasheni, ni uhai. Helemu inalinda kichwa na koti linakuepusha na ajali pamoja na baridi kali inayoweza kukuletea maradhi baada ya muda,” alisema Maganga.
Aidha, aliwasisitiza bodaboda kuzingatia sheria kila wakati, kuwaheshimu watumiaji wengine wa barabara kama waenda kwa miguu na waendesha baiskeli, pamoja na kutoa nafasi kwa magari ya dharura kama ambulensi, magari ya zimamoto na ya polisi.
Maganga alionya pia dhidi ya tabia ya kubeba mizigo mikubwa pamoja na abiria kwenye pikipiki moja, akieleza kuwa kitendo hicho hupunguza usalama na kuongeza hatari ya ajali.
“Pikipiki inapaswa kubeba mtu mmoja pekee. Mzigo mkubwa upelekwe kwa usafiri unaofaa. Usalama siyo bahati — ni uamuzi wa dereva,” alisisitiza.
Alimalizia kwa kuwataka madereva hao kuwa mabalozi wa usalama barabarani kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe, abiria na jamii kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED