Dk. Mpango aitaka Wizara ya Afya kuunganisha mifumo na Serikali Mtandao

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:51 PM Sep 03 2025
Dk. Mpango aitaka Wizara ya Afya kuunganisha mifumo na Serikali Mtandao.
Picha: Mpigapicha Wetu
Dk. Mpango aitaka Wizara ya Afya kuunganisha mifumo na Serikali Mtandao.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha mifumo yake inasomana na ile ya Serikali Mtandao (eGA) ili kurahisisha utoaji wa huduma, hususan matibabu ya wagonjwa wa saratani.

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kituo mahiri cha mafunzo ya Saratani na kituo cha upandikizaji figo kitakachogharimu Sh bilioni 30.4, Dk. Mpango pia alisisitiza umuhimu wa utoaji elimu kuhusu saratani na magonjwa yasiyoambukiza kuanzia ngazi ya shule ya msingi.

“Kwa sasa tuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi, tezi dume, matiti na mengineyo, hali inayosababisha vifo kutokana na kuchelewa kugundulika. Tukiboresha mifumo hii na ikasomana, itarahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi na hivyo wagonjwa watatibiwa mapema,” amesema Dk. Mpango.

Aidha, ameahidi kuwa serikali italifanyia kazi ombi la Sh bilioni 13.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya saratani na Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya huduma za figo, akibainisha kuwa magonjwa hayo yamepewa kipaumbele cha kitaifa.

Ameongeza kuwa Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH) imekuwa mstari wa mbele katika kupunguza changamoto za matibabu, ikiwemo kutoa huduma za kibingwa za figo. “Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya vifaa tiba na kujenga vituo vya utoaji wa matibabu ili kupunguza changamoto za wananchi katika maeneo mbalimbali,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH), Profesa Abel Makubi, amesema hospitali hiyo kwa sasa inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma bobezi 17, hatua iliyopunguza kwa asilimia 80 idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipewa rufaa kwenda hospitali nyingine au nje ya nchi.

“Tunaishukuru serikali kwa kuwekeza katika sekta ya afya, jambo lililosababisha mafanikio makubwa. Huduma tunazotoa ni pamoja na upandikizaji uloto, upasuaji wa mishipa ya damu, upasuaji wa moyo kwa njia ya matundu na huduma nyingine nyingi za kibingwa,” amesema Prof. Makubi.

Ameongeza kuwa kuzinduliwa kwa kituo cha mafunzo ya saratani pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la kituo hicho kutapanua wigo wa huduma za kibingwa nchini.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Seif Shekalaghe, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, amesema mafanikio makubwa ya Hospitali ya BMH ni matokeo ya uwekezaji wa serikali na jitihada za wizara katika kusimamia sekta ya afya.