Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umeendeleza maono aliyoacha Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kupamba na ujinga, maradhi na umaskini.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni moja ya viongozi ambao amevipiga vizuri vita hivyo kwa kuonesha kwa vitendo, kuuenzi na kuuthamini urithi wa Baba wa Taifa.
Amesema hayo leo Oktoba 14 wilayani Mkalama mkoani Singida wakati akihutubia wananchi ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Balozi Dk. Nchimbi amesema Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume ndio waliounganisha nchi yetu kuwa taifa moja.
Amesma: "Ndiyo, mwasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baba wa Taifa ndio aliyeanzisha falsafa inayotumika pamoja siku ya leo. Falsafa ya kuliunganisha taifa letu kuwa taifa moja lenye umoja, amani na mshikamano".
Amesema Hayati Nyerere ni mwanasiasa na kiongozi aliyesimamia usawa, utu na upendo. Lakini vile vile alianzisha sera ya ujamaa na kujitegemea ambayo iliwahamasisha wananchi kushirikiana, kuheshimiana na kutanguliza maslahi ya taifa letu mbele.
Amesema leo Watanzania watafanya makosa sana kama wataiacha misingi ya umoja, mshikamano na amani aliyoipigania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED