Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, serikali yake itagawa mitungi ya gesi bure kwa Watanzania wote kama sehemu ya mpango wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza leo, Oktoba 15, 2025, katika mikutano yake ya kampeni mkoani Kilimanjaro, Doyo amesema hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa mkaa unaochangia uharibifu mkubwa wa mazingira na misitu kutokana na ukataji wa miti ovyo.
“Serikali yangu itahakikisha kila kaya inapata mtungi wa gesi bure, ili Watanzania wote watumie nishati safi badala ya mkaa unaoharibu mazingira yetu,” amesema Doyo.
Ameongeza kuwa, ili kufanikisha mpango huo, serikali ya NLD itapunguza kodi kwa wawekezaji wa sekta ya gesi, hatua itakayowezesha kampuni nyingi zaidi kushiriki katika utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Doyo, mpango huo utasaidia pia kupunguza bei ya gesi nchini, jambo litakalowezesha kila familia kumudu gharama za matumizi ya gesi na hivyo kuboresha afya na ustawi wa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED