Mahakama Kuu Zanzibar yatupilia mbali kesi ya Hamad Masoud dhidi ya ZEC

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 08:25 PM Oct 15 2025
Mahakama Kuu Zanzibar yatupilia mbali kesi ya Hamad Masoud dhidi ya ZEC.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mahakama Kuu Zanzibar yatupilia mbali kesi ya Hamad Masoud dhidi ya ZEC.

Mahakama Kuu ya Zanzibar imekataa Ombi la kikatiba Namba 2 la mwaka 2025 lililofunguliwa na Hamad Masoud wa Chama cha CUF, ambaye alikuwa akipinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa kutomteua kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Hukumu hiyo iliyosomwa kwenye Mahakama Kuu Tuguu Zanzibar, imesema kuwa mlalamikaji alipewa nafasi ya kutosha ya kusikilizwa kabla ya kuondolewa kwenye orodha ya wagombea, hivyo Tume haikukiuka taratibu za kisheria.

Jaji wa Mahakama Kuu, Ibrahim Mzee Ibrahim, alisema kuwa ushahidi uliowasilishwa na mawakili wa Serikali na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) unaonyesha kuwa Tume ilifuata masharti yote ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, na hoja za mlalamikaji hazina msingi wa kikatiba.

“Mahakama imejiridhisha kuwa mlalamikaji alipewa haki ya kujieleza, na maamuzi ya Tume yalitolewa kwa mujibu wa sheria. Kwa hivyo, ombi hili linatupiliwa mbali,” alisema Jaji Ibrahim.