Serikali kuja na mkakati kudhibiti vifaa vinavyotumia umeme mwingi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:41 PM Oct 15 2025
news
Picha Maulid Mmbaga
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga.

SERIKALI imesema kuanzia sasa kutakuwa na utaratibu maalumu wa kukagua na kujiridhisha juu ya ubora wa vifaa vyote vya umeme vitakavyoingiozwa nchini katika kuhakikisha kwamba vina ufanisi unaotakiwa wa matumizi sahihi ya nishati ua umeme.

Pia imeelezwa kuwa vifaa vyote vya umeme uvitakavyoruhusiwa kutumika nchini ni lazima vitatakiwa kuwa na viwango vya ubora na ufanisi wa matumizi ya umeme vitakavyopendekezwa na kwamba wananchi watavijua kupitia nembo ya Shirika la viwango Tanzania (TBS).

Hayo yalibainishwa leo mkoani Dar es Salaam na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga, wakati akizungumzia uzinduzi wa maabara ya kwanza nchini itakayotumika kupima ubora na ufanisi wa vifaa vya umeme vitakavyoingizwa nchini.

“Zimekuwa zikifanyika jitihada mbalimbali katika kuhakikisha tunapunguza upotevu wa umeme ambako mwaka 2020 ulikuwa takribani asilimia 20, na sasa umepungua hadi 14, lakini matarajio yetu kutokana na hatua hizi za kuhakikisha ufanisi wa vifaa kiwango cha upotevu kishuke hadi asilimia tisa,” alisema Mhandisi Luoga.

Amesema serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wamekuwa wakitekeleza mradi wa matumizi sahihi ya umeme, na kwamba kesho ‘leo’ kutakuwa na uzinguzi wa viwango fanisi vya nishati, pamoja na uanzishwaji wa maabara ya upimaji ufanisi wa vifaa vinavyotumia umeme.

Pia amesema hatua hiyo ni muhimu kwa Tanzania kwasababu wanaenda kuangalia upimaji wa vifaa vinavotumia umeme, na kwamba lengo ni kuhakikisha vifaa vinavyotumia nchini vinatumia nishati kwa ufanisi, ili kupunguza gharama kwa watumiaji, na kulinda mazingira zidi ya uzalishaji wa hewa ukaa.

Aidha, ameeleza kuwa juhudi hizo zitasaidia umeme wa ziada kwenye gridi ya taifa kutumika kwenye maeneo mengine ya nchi yenye upungufu, akisema hatua za kudhibiti ubora wanaenda kutumia nishati hiyo kwa njia nzuri na sahihi.

“Kupitia mradi huu Tanzania inaenda kuzindua viwango vya kwanza vya chini ya matumizi ya nishati ya umeme, kwa vifaa vitano vyenye matumizi makubwa ikiwemo viyoyozi, majokofu, luninga, feni na mota za umeme, ili kuwawezesha Watanzania kutambua ubora wake,” amesema Mhandisi Luoga.

Akitolea mfano wa jokofu, amesema mengi yaliyoko sokoni yana nyota tano na kwamba katika ubora yametofautiana kutokana na nyota iliyotikiwa.

“Ukiona limetikiwa kwenye nyota ya kwanza jua uwezo wake inaweza kugandisha kitu kwa saa tano, na ubora unaenda kwa mtiririko huo na ukiona limetikiwa kwenye nyota ya tano jua linaweza kugandisha kwa saa moja hivyo utatumia umeme mgodo,” amesema.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wizara inaandaa viwango katika teknolojia ya kupikia kwa kutumia nishati safi, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia wa miaka 10, akisema serikali inaendelea kuhamashisha jamii kuzingatia kutumia vifaa vyenye ubora.

Amesema uanzishwaji wa maabara hizo unalenga kuimarisha utekelezaji wa sera ya taifa ya 2015 inayozungumzia matumizi bora ya nishati, pamoja na Dira ya Maendeleo 2050, akisema hatua hiyo pia itasaidia kuondoa mzigo kwenye gridi ya taifa na kusaidia taifa kuwa na umeme unaokidhi mahitaji.

“Pia maabara hizi zitasaidia Watanzania kutumia umeme kidogo kwa ufanisi uleule na kuchochea ushindani wa viwanda vya ndani kwa kutengeneza vifaa vyenye viwango na ufanisi,” amesema Mhandisi Luoga.

Msadidizi wa Mwakilishi Mkazi wa UNDP Gertrude Lyatuu
Msadidizi wa Mwakilishi Mkazi wa UNDP Gertrude Lyatuu, amesema hatua za kupima ubora na ufanisi wa vifaa vinavyotumia umeme utasaidia kupunguza uhitaji mkubwa wa umeme, gharama za matumizi, na kuongeza ufanisi wa maisha kwa Watanzania.

Naye, Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya (EU), amesema hatua iliyofikia Tanzania ni ukurasa mkubwa wa kuchagiza maendeleo kwakuwa kwa miaka mnne iliyopita walikutana na serikali pamoja na UNDP na kuangalia ni namna gani nzuri ya kumalicha changamoto ya matumizi makubwa ya umeme.

Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya (EU).
“Matumizi sahihi ya umeme ni njia sahihi ya kupata nishati nyingi zaidi na inasaidia kukidhi mahitaji ya idadi ya watu inayoendelea kuongezeka kila siku,” amesema Stalmans.