RC Malisa: Waajiri wasilisheni michango ya wanachama NSSF kwa wakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:44 PM Oct 15 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
WaWafanyakazi na wanachama wa Mfuko wa NSSF.

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amewataka waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanatimiza takwa la kisheria la kuwasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ili kuendelea kuboresha ustawi wa wafanyakazi wao na kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii nchini.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa majiko ya nishati safi kwa baadhi ya mama na baba lishe, wanachama wachangiaji wa mpango wa hiari na wastaafu wa Mkoa wa Mbeya, yaliyotolewa na NSSF.

Malisa amesema hatua ya kuwasilisha michango kwa wakati ni muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi, akisema kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu wa kisheria na ni sehemu ya kuwajali wafanyakazi, kama wanavyosema NSSF kwamba ‘wanapaka rangi ustaa wao’ kupitia mafao wanayonufaika nayo.

“Niwasisitize wananchi waliojiajiri, wakiwemo vijana na wajasiriamali wadogo, kujiunga na kuchangia katika mpango wa hifadhi ya jamii wa NSSF ili kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu, uzazi, uzee na mirathi. 

“Pia niipongeza NSSF kwa kuunga mkono ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya matumizi ya nishati safi, hatua hiyo ni ushahidi wa dhahiri wa dhamira ya mfuko katika kugusa maisha ya wananchi kwa vitendo,” amesema. 

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema utoaji wa majiko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya mfuko ya kurudisha kwa jamii ambayo inalenga kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.