Kyara: Nitajenga miradi ya maji kila kata

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 06:09 PM Oct 15 2025
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majaliwa Poul Kyara.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majaliwa Poul Kyara.

Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majaliwa Poul Kyara, amewataka wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kufanya mabadiliko ya kweli kwa kuchagua chama hicho, akisisitiza kuwa wakati umefika wa kujikomboa kiuchumi na kijamii.

Akizungumza leo katika moja ya mikutano yake ya kampeni mkoani Arusha, Kyara, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi, serikali yake itahakikisha upatikanaji wa bima za afya kwa wananchi wote, pembejeo za kilimo kwa bei nafuu, na elimu bora bure kwa wanafunzi nchini.

“Tutahakikisha kila kata nchini inapata majisafi na salama, kwa sababu huduma ya maji ni haki ya msingi, si anasa,” amesema Kyara .

Aidha, ameahidi kuwa mkoa wa Arusha utapata standi ya kisasa ya mabasi, sambamba na kuboresha huduma za usafiri na miundombinu kwa ujumla.

Katika sera zao, chama cha SAU kimeeleza dhamira ya kuwasaidia wakulima na wafugaji kwa kuondoa changamoto za masoko na kuwezesha uongezaji thamani wa mazao na bidhaa za mifugo, hatua itakayoongeza ajira na kipato kwa wananchi.

Kwa upande wake, Saimon Bayo, mgombea Ubunge wa chama hicho katika Mkoa wa Arusha, amesema Arusha si “shamba la bibi” na hivyo ni wakati wa wakazi wa mkoa huo kuchagua viongozi wazawa watakaosukuma mbele maendeleo ya eneo hilo.

Bayo, ametaja teknolojia, kilimo na elimu kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu, akiwataka wananchi kumpa ridhaa ili kuleta mabadiliko makubwa ndani ya mkoa huo.

Katika kampeni zake mkoani Arusha, wagombea hao wa SAU wametembelea majimbo ya Arusha Mjini, Arumeru Magharibi na Arumeru Mashariki, wakijipatia uungwaji mkono kutoka kwa wananchi.