Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kukuza na kuendeleza zao la kahawa kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT), sambamba na kuimarisha sekta ya uvuvi katika Ziwa Victoria kwa kudhibiti uvuvi haramu.
Akizungumza leo, Oktoba 15, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Muleba, Dk. Samia amesema serikali yake itaendelea kuwasaidia wakulima wa kahawa ili kuongeza tija na kipato chao kupitia mpango huo wa BBT unaolenga kuinua sekta ya kilimo nchini.
Amesema pia kuwa serikali itatoa boti za uvuvi, boti za kubeba wagonjwa, na boti za doria kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu ambao umekuwa ukisababisha kupungua kwa samaki katika Ziwa Victoria.
“Kuna changamoto kubwa ya wagonjwa kushindwa kusafirishwa kwa wakati, hasa kwa wakazi wa visiwa,” alisema Dk. Samia, akibainisha kuwa serikali yake italeta boti mbili za kusafirisha wagonjwa kwa kata za Goziba na Bumbire, pamoja na kujenga gati mbili katika vijiji viwili vitakavyotajwa.
Aidha, ameahidi kutoa boti tatu za doria kwa ajili ya kulinda usalama wa wavuvi na kudhibiti uvuvi haramu, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa samaki na kulinda rasilimali za Ziwa Victoria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED