Samia: Nitaleta boti tano za wagonjwa, usalama Kagera

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:31 PM Oct 15 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amewaahidi wananchi wa Kagera kupeleka boti tano zitakotumika kuimarisha usalama na kusafirisha wagonjwa.

Pia, Dk Samia amefafanua kuwa boti hizo zitatumika katika kudhibiti uvuvi haramu, unaosababisha upungufu wa samaki katika Ziwa Victoria.

Katika ya ahadi hiyo, Dk Samia amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kama ambavyo wanavyojitokeza kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni zake katika maeneo mbalimbali.

Dk Samia ametoa ahadi hiyo, leo Jumatano Oktoba 15,2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Muleba mkoani Kagera ikiwa ni siku ya kwanza tangu atue mkoani humo, akitokea Geita.

Akizungumzia suala la usafiri na usafirishaji wa mazao ya uvuvi na kilimo katika Ziwa Victoria, Dk Samia ameahidi kuishughulikia changamoto hiyo, pamoja na ile usafirishaji wa wagonjwa kwa wakati katika visiwa vya Ziwa Victoria.

“Miongoni mwa ahadi zetu mkitupa ridhaa,mbele tunakoendelea hapa Muleba tutaleta boti mbili za kusafirisha wagonjwa kata za Gozib ana Bumbile, sambamba na kujenga gati mbili vijiji vya Kituo na Mrumo,”

“Tutajenga hizi gati, ili hizi boti zipate eneo la kupakia na kushusha, lakini tutaleta boti tatu za doria kwa ajili ya kuimarisha usalama na doria, udhibiti wuvuvi haramu unaochangia upungufu wa samaji katika ziwa Victoria,” ameeleza Dk Samia.

Sambamba na hilo, Dk Samia ameahidi kuongeza uzalishaji wa miche ya kahawa na kuwezesha upatikanaji wa matrekta kwa ajili ya wakulima wa kahawa mkoani humo.

“Tutaendelea kuboresha huduma za afya na elimu ili kutoa fursa kwa vijana wetu kusoma kadri Mungu atakavyowajalia, hatua itakayorahisisha safari yao ya elimu,”

“Tutawekeza zaidi ufugaji wa njia ya vizimba, ili vijana wafuge samaki kwa njia ya kitalaamu watakaochakatwa kwenye viwanda tutakavyoviweka,” amesema Dk Samia na kuongeza kuwa.

“Niwaahidi mkitiki vema Oktoba haya yote tunakwenda kushughulikia nayo,” amesisitiza Dk Samia.

Tujitokeza Oktoba 29.

“Tumuombe Mungu Oktoba 29, tuamke salama na furaha, baba, mama unapotoka nyumbani hakikisha vijana wako waliojindikisha waende na wewe kupiga kura,”

“Lakini haitakuwa na maana wingi huu kwenye viwanja, halafu kukawe na upungufu kwenye masanduku, niwaombe sana ndugu zangu tumejaza viwanja, twendeni tukajaze masanduku,” amesema.