Walimu wanawake Pwani wapatiwa mafunzo ya ujasiriamali

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 09:00 PM Oct 15 2025
Picha katika matukio kwenye mafunzo ya Ujasiriamali kwa walimu wa kitengo cha wanawake.
Picha: Mpigapicha Wetu
Picha katika matukio kwenye mafunzo ya Ujasiriamali kwa walimu wa kitengo cha wanawake.

Kitengo cha Walimu Wanawake wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Pwani kimeandaa mafunzo maalumu kwa viongozi na wajumbe wake kutoka kila wilaya, yakiwajengea uwezo wa kujipatia kipato kupitia ujasiriamali na kutambua wajibu wao katika nafasi za uongozi.

Mwenyekiti wa kitengo hicho, Sharifa Mngwali, amesema Oktoba 14 mjini Kibaha kuwa kila mwalimu anatakiwa kuanza kufanya ujasiriamali kabla ya kustaafu ili kujiepusha na changamoto za maisha ya baadaye.

“Ni muhimu kwa kila mwalimu kuwa na shughuli za ziada za kiuchumi ili kuepuka ugumu baada ya kustaafu,” amesema Mngwali.

Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susan Shesha, ameipongeza kitengo hicho kwa jitihada za kuandaa mafunzo hayo na akasisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano miongoni mwa walimu ili kuendeleza maendeleo ya kiuchumi. Aidha, Shesha aliwataka viongozi wa kitengo cha wanawake kuhamasisha jamii kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Eda Michael, amesema kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kuondokana na utegemezi wa mshahara pekee na pia kupunguza uraibu wa mikopo michache isiyofaa ambayo wengi wao wamekuwa wakikopa.

Walimu hao walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali, ikiwemo mbinu za kutangaza bidhaa zao kwenye maeneo mbalimbali, yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka ndani ya kitengo hicho, kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kuboresha maisha yao.