John Mrema: CHAUMMA hatutaki bunge kibogoyo, goigoi na la wapigamakofi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:53 PM Oct 14 2025

 Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), John Mrema.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), John Mrema.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), John Mrema, amesema endapo chama hicho kitashika dola baada ya uchaguzi wa mwezi huu, kitaunda bunge lenye nguvu, huru na linaloisimamia serikali kwa uwajibikaji wa kweli.

Akizungumza leo katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CHAUMMA, Salum Mwalimu, Mrema amesema chama hicho hakitaki bunge “kibogoyo” linaloshindwa kuwawakilisha wananchi, bali linataka bunge lenye uwezo wa kupaza sauti za wananchi na kuhoji utendaji wa serikali.

“CHAUMMA hatutaki bunge la wapiga makofi, bunge kibogoyo. Tunataka bunge ambalo siyo kigoigoi, bali bunge huru linalotetea kero za wananchi wake,” amesema Mrema.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa ilani ya chama hicho ukurasa wa 10, bunge ni mhimili muhimu wa kusimamia serikali, hivyo wabunge wa CHAUMMA watapewa uhuru kamili wa kutoa maoni, kuuliza maswali na kuibua hoja kwa niaba ya wananchi bila kuingiliwa.

“Serikali itawapa uhuru wabunge kutoa maoni kwa niaba ya wananchi wanaowawakilisha. Tunataka mbunge awe sauti ya wananchi. Kabla ya kwenda bungeni, afanye mikutano na wananchi ili wampatie mawazo na kero zao,” amesisitiza Mrema.

Mrema ameitimisha kwa kusisitiza kuwa lengo la CHAUMMA ni kuhakikisha bunge linarejesha heshima na mamlaka yake ya kikatiba kama chombo kinachojitegemea na kusimamia vyema uwajibikaji wa serikali.