Zaidi ya abiria 700 wakwama Dodoma baada ya treni kupata ajali Kintinku

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 08:38 PM Oct 15 2025
Zaidi ya abiria 700 wakwama Dodoma baada ya treni kupata ajali Kintinku
Picha: Mpigapicha Wetu
Zaidi ya abiria 700 wakwama Dodoma baada ya treni kupata ajali Kintinku

Zaidi ya abiria 700 waliokuwa wakisafiri na treni ya reli ya kati kuelekea mikoa ya Tabora, Mpanda na Kigoma wamekwama kwa zaidi ya saa 18 katika Stesheni ya Dodoma baada ya treni ya matengenezo kupata ajali eneo la Kintinku, wilayani Manyoni mkoani Singida.

Hali hiyo imewalazimu abiria hao kufanya maandamano hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kufikisha malalamiko yao kutokana na kushindwa kupata huduma muhimu na maelezo kuhusu safari yao.

Abiria hao walifika Dodoma jana saa 2:00 usiku, lakini walilazimika kusubiri hadi leo majira ya saa 8:00 mchana kabla ya kuanza safari yao kuelekea mikoa ya Tabora, Mpanda na Kigoma.

Ashura Madaraka, mmoja wa abiria, amesema:
 "Tangu tumekwama hapa jana saa mbili usiku tukaambiwa tutaanza safari saa 7:00 usiku, lakini hatukuondoka muda huo. Leo asubuhi saa 1:00 ndipo masta alifika kutuambia tutaendelea. Tunataka kujua tutabaki hapa hadi lini, kwani huduma muhimu kama choo hazipo au ni za kulipia."

Imani Sadiki, abiria mwingine, amebainisha changamoto zinazowakumba kutokana na kukosa huduma za msingi.
 "Hapa wanasema choo ni cha kulipia, hatuwezi kuelewa kwa nini tunapaswa kulipa 500 shilingi wakati hatukujiandaa kwa hali hii. Pia chakula shirika linasema kitagharamiwa, lakini huduma zingine bado hazipo," amesema.

Abiria hao wamelazimika kuandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa kufikisha kilio chao, huku akisisitiza kuwa miongoni mwao wapo watoto wadogo ambao hawawezi kuvumilia adha hiyo.

Stesheni Masta wa Dodoma, Festo Mgomapayo, alikiri tukio hilo na kusema:
 "Kweli abiria hawa wamekwama hapa tangu jana majira ya saa mbili usiku kutokana na ajali ya treni ya matengenezo eneo la Kintinku wakati ikielekea mkoa wa Tabora."