'Hakuna hofu kuhusu huduma, dawa ARVs'

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 06:32 PM Apr 09 2025
Dawa
Picha: Mtandao
Dawa

SERIKALI imesema itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania atakayekosa huduma hizo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema hayo leo, Aprili 9, Bungeni jijini Dodoma, wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema serikali inatambua mabadiliko ya sera za misaada kutoka kwa baadhi ya wafadhili wa muda mrefu wa masuala ya UKIMWI.

Majaliwa, amesema kutokana na hali hiyo serikali imechukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye eneo la utaoji huduma kwa WAVIU.

“Hatua hizo zenye lengo la kuwezesha Taifa letu kujitegemea zitaendelea kuchukuliwa pia katika maeneo mengine.Niwahakikishie Watanzania wote, kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania atakayekosa huduma hizo,” amesema.