Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema chama hicho hakihitaji kushinda uchaguzi kutokana na migogoro ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), bali kinataka ushindi wa haki unaotokana na ridhaa ya wananchi.
Akizungumza jijini Mwanza jana, Heche alisema amekuwa akipigiwa simu mara kwa mara, hasa baada ya kutangazwa kwa majina ya wagombea ubunge kupitia CCM, ambapo baadhi ya watu wamependekeza CHADEMA itumie vurugu na migawanyiko ndani ya chama hicho tawala kama fursa ya kupata viti vingi bungeni.
“Kuna watu wengi jana na leo wamenipigia kuhusu yanayoendelea kwenye teuzi za CCM. Wengi walisema kutokana na vurugu, kuumizana, migogoro, maumivu na chuki zilizopo ndani ya CCM, hii ilikuwa fursa kwetu kupata wabunge wengi kama CHADEMA,” alisema Heche.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa CHADEMA haitaki kushinda kwa misingi hiyo, akibainisha kuwa lengo lao ni kupata ushindi halali unaotokana na imani na uamuzi wa wananchi.
“Sisi hatutaki kushinda uchaguzi kwa sababu CCM wamegombana. Hatutaki wabunge bungeni kwa sababu wabunge wa CCM wameumizana au kwa chuki zao wakakimbilia kwetu. Tunachotaka ni kushinda uchaguzi kwa haki,” aliongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED