INEC yaridhia Bariadi kugawanywa majimbo mawili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:38 PM Apr 25 2025
news
INEC
Tume Huru ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imejiridhisha na kauli moja ya wadau wa Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu ligawanywe kuwa na majimbo mawili ya Bariadi Mjini na Bariadi Vijijini, ikiwa ni baada ya uongozi kutembelea na kujionea hali halisi.

Taarifa ya INEC iliyotolewa leo Aprili 25,2025, imeeleza kuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele, ametembelea jimbo hilo na kuzungumza na wadau wa Halmshauri ya Mji wa Bariadi na Halmshauri ya Wilaya ya Bariadi, na kujiridhisha kama ombi la kuligawa lililowasilishwa kupitia Katibu Tawala Mkoa ni la kweli na lilifuata mchakato wote kwa mujibu wa sheria.

Jaji Mwambegele amesema baada ya mchakato huo wa kujiridhisha INEC itakutana na kutoa majibu ya majimbo yote yaliyoomba kugawanywa au kubadili majina kama yamekubaliwa au la.

Mapema wakati wa majadiliano wadau wa uchaguzi kutoka Wilaya ya Bariadi waliiambia INEC kuwa wamekubaliana kwa pamoja kuligawa Jimbo la Bariadi na kutoa majimbo mawili ya Bariadi Mjini na Bariadi Vijijini ili kurahisisha shughuli za maendeleo wilayani humo.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, viongozi wa Wilaya ya Bariadi, viongozi wa vyama vya siasa Bariadi, wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake, vijana, wenye ulemavu na wazee wa Kimila.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipokea mapendekezo kuanzia Februari 27, 2025 hadi Machi 26, 2025.

“Vigezo vinavyohusika katika ugawaji wa majimbo kuwa ni pamoja na hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya muungano, uwezo wa ukumbi wa Bunge; na  idadi ya viti maalum vya wanawake,”amesema.