Watendaji wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wa mikoa ya Mbeya na Songwe, wametakiwa kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu kwa kufuata sheria na miongozo ili kuepuka kuwa chanzo cha vurugu wakati wa uchaguzi.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa INEC, Mtibora Selemani ameyasema hayo jijini Mbeya wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo, Maofisa Uchaguzi na Maofisa Ununuzi wa mikoa ya Mbeya na Songwe.
Amewataka maofisa hao kuwapatia ushirikiano wadau mbalimbali wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa na waangalizi wa uchaguzi kwa kuzingatia mipaka ya kisheria ili kuondoa malalamiko na vurugu kwenye kazi hiyo.
“Tume imewateua kutokana na uchapakazi, uadilifu na uzalendo wenu, kwahiyo mnakwenda kufanya kazi kwa niaba ya tume, hakikisheni mnazingatia sheria ili kazi hiyo ifanyike kwa ufanisi,” amesema Selemani.
Vilevile amewataka maofisa hao kuajiri wasaididi amba oni waadilifu ili kuepuka kusababisha matatizo na kwamba endapo uchaguzi utaharibika maofisa hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED