KASI ya matumizi ya shisha Zanzibar yatajwa kuongezeka hasa kwa vijana jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
Meneja wa kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar, Omar Muhammed Suleiman,amesema kuwa shisha ni kichocheo kikubwa cha maradhi yasiyoambukiza.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akiwasilisha mada ya maradhi yasiyoambukiza katika mafunzo kuhusu maradhi yasiyoambukiza kwa waandishi wa habari visiwani Zanzibar ambayo yameandaliwa na Shirikisho la Maradhi Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) kwa kushirikiana na shirikisho la maradhi yasiyoambukiza Zanzibar.
Alisema shisha ni hatari kwa afya na ndani yake kuna kemikali nyingi ambazo ni hatari kwa maisha ya binadamu na uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 kwa siku.
"Ikiwa uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya inasababisha saratani,kuharibu mapafu,figo,ubongo jiulize athari ambazo unazipata kupitia kwenye shisha,mtumiaji wa shisha maisha yake yapo hatarini sana"alisema.
Alisema athari za shisha kiafya ni nyingi ikiwemo kupoteza nguvu za kiume na huathiri nguvu za kizazi kwa wanaume na wanawake.
Katika kumbi za starehe shisha inavutwa kwa kutumia mirija maalum(Filta) ambao kila mtumiaji huwa na mrija wake na hupokezana katika kuvuta.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED