Kesi ya kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi inatajwa leo katika Mahakama Kuu, Masijala Kuu ya Dodoma, ambapo shauri hilo linasikilizwa kwa njia ya mtandao. Shauri hilo linahusu malalamiko yaliyowasilishwa na Mgombea Urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, akipinga uamuzi wa Tume kuzuia urejeshaji wa fomu za uteuzi.
Hata hivyo, baada ya pande zote kuwasilisha hoja zao, Mahakama ilitoa pingamizi na kuelekeza kuwa kesi ya msingi isikilizwe kwanza kwa haraka na kwa maandishi. Vilevile, Mahakama imeiagiza Serikali kuandaa majibu yake, huku pande zote zikielekezwa kukutana tena Jumatatu saa nane mchana katika Masijala Kuu Dodoma, kwa ajili ya kupitia mashauri na kupanga tarehe ya kutolewa kwa maamuzi.
Mgombea wa urais wa chama hicho, Luhaga Mpina, amesema hoja walizowasilisha ni nzito na anaamini watashinda. Amefafanua kuwa Tume ya Uchaguzi ilitoa kanuni zinazoeleza utaratibu wa urejeshaji fomu, lakini hakuna kipengele kinachomzuia mgombea kurejesha fomu. Kwa mujibu wake, hatua hiyo haijawahi kutokea nchini na inaashiria uonevu mkubwa.
Mpina amewataka wabunge na madiwani wa chama chake kuendelea na kampeni bila hofu, akisisitiza kuwa kila changamoto itatatuliwa. Aidha, alisema chama chao kitaibuka na ushindi wa zaidi ya asilimia 70, huku akifichua kwamba licha ya kuombwa na Katibu Mkuu wa chama chake kurejea CCM, hawezi kufanya hivyo.
“Naomba Mahakama iondoe kikwazo hiki haraka ili niendelee na kampeni za mwisho dhidi ya CCM, nikiwa majukwaani na katika uchaguzi,” amesema Mpina.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED