Mgombea ubunge ACT Morogoro aahidi kupambana na ushoga

By Christina Haule , Nipashe
Published at 04:40 PM Aug 25 2025
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Jamali Saidi

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Jamali Saidi, ameahidi kushughulikia changamoto tatu kuu endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo, ikiwemo kupambana na mmomonyoko wa maadili kwa vijana.

Akizungumza leo mara baada ya kuchukua fomu za kugombea Ubunge katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Manispaa ya Morogoro, Jamali amesema moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha vijana wanajiepusha na vitendo vya ushoga, uhalifu na ubakaji, na badala yake kuelekezwa kwenye fursa za ajira.

“Vijana wetu wamebadilika sana, wanaendekeza vitendo visivyofaa. Nikichaguliwa nitahakikisha hali hii inakomeshwa na vijana wanajikita kwenye shughuli za kujiletea maendeleo,” amesema Jamali.

Aidha, ameahidi kutenga mpango maalumu wa kuwasaidia wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 kwa kuwapatia chakula kila mwisho wa mwezi sambamba na kuwahakikishia upatikanaji wa bima ya afya.

Jamali amesema sera hizo zitakuwa sehemu ya mikakati yake ya kuhakikisha maendeleo ya wananchi wa Morogoro Mjini yanaboreshwa kwa vitendo na sio kwa ahadi pekee.