MLINZI Daniel Mwangaya (32) amehukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumua mkewe Pili Musa kwa kumkata kwa panga mwilini kutokana na wivu wa mapenzi.
Pili alidai kuwa aliporejea nyumbani saa mbili usiku alimkuta mumewe anapika chakula na baada ya muda alimweleza kuwa anatoka mara moja kuna kitu muhimu amesahau nyumbani kwao, hivyo anakwenda kukichukua.
Wakati anaondoka, mumewe alimfuata nyuma bila yeye kufahamu na kuanza kumkata kwa panga sehemu za mwili wake, akaanguka chini barabarani, akamchukua na kuanza kumburuza hadi kumtumbukiza kwenye shimo refu.
"Akaanza kunipiga na mawe kisha akaniacha ndani ya shimo, akarudi nyumbani kwake, shimo hili lilikuwa limechimbwa katika shamba la jirani yangu na lilikuwa limejengewa," alidai Pili.
Ilidaiwa kuwa siku iliyofuata ambayo ilikuwa Jumamosi, mshtakiwa alikwenda eneo hilo na kumkuta mkewe yumo ndani ya shimo akiwa hai, akamwuliza "kumbe hujafa" ndipo alichukua ngazi na kushuka shimoni akaanza kumchoma kwa kisu tumboni.
Mshtakiwa alipomaliza kumchoma, alikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti kuwa mkewe amepotea na siku iliyofuata asubuhi alikwenda tena kwa Mwenyekiti kutoa taarifa kuwa mkewe hajaonekana.
Baada ya nusu saa, siku hiyo alikwenda tena kwa Mwenyekiti kutoa taarifa kuwa amepata taarifa mkewe amekutwa ndani ya shimo katika shamba la jirani yao.
Siku hiyo ya Jumapili alipita mchunga ng'ombe, eneo hilo akasikia sauti ya mtu akiomba msaada ndipo alisogea eneo hilo, kuona mtu ndani ya shimo. Alikwenda kwa majirani akatoa taarifa wakamsaidia kumtoa ndani ya shimo akapelekwa hospitalini.
Akitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Hakimu Mkazi Mkuu Romuli Mbuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, alisema kuwa kutokana na mshtakiwa kukiri kosa mwenyewe, anamhukumu kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani.
Mshtakiwa alikiri kosa hilo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.
"Kwa sababu mshtakiwa umekiri kosa mwenyewe, mahakama inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani," alisema Hakimu Mbuya.
Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Erick Kamala aliomba mahakama itoe adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hizo.
Baada ya Wakili Kamala kudai hayo, mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ni wivu wa mapenzi uliomsukuma kutenda kosa, ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana familia ya watoto wawili, mke na wazazi wanamtegemea.
Mwanganya alitenda kosa hilo Septemba 2024 eneo la Bunju A, Gosheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam baada ya mkewe kurudi nyumbani saa mbili usiku akiwa anatoka matembezi na watoto wake wawili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED