Wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameanza kunufaika na uboreshaji wa miundombinu kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), unaotekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.
Akielezea manufaa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, amesema awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 10.01 kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa ofisi ya wahandisi itakayotumika kama maabara. Utekelezaji huo unafanywa na mkandarasi M/S CHINA SICHUAN INTERNATIONAL COOPERATION CO LTD kwa gharama ya shilingi bilioni 22.27.
Amesema awamu ya pili inalenga kuboresha hali ya uchumi wa mji kwa kuongeza mapato ya halmashauri na wananchi kwa ujumla, ambapo tayari mkandarasi amepatikana kwa ajili ya ujenzi wa masoko makubwa mawili ya kisasa ya Manzese “A” na Manzese “B”. Masoko hayo yatabeba wafanyabiashara wengi zaidi na yatajumuisha maduka ya kawaida, maduka ya kifedha, maghala pamoja na kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka kwa gharama ya shilingi bilioni 22.9.
“Masoko haya yanakwenda kuongeza mapato ya halmashauri karibu bilioni 2. Kwa sasa tunakusanya bilioni 9 lakini ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tunakusanya shilingi bilioni 11 kwa mwaka. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za kutekeleza miradi hii. Pia nawaasa wananchi kutumia miundombinu hii kwa ufasaha, kuilinda na kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu,” amesema Muhoja.
Kwa upande wake, Mhandisi Nicholaus Danda, Mratibu wa mradi wa TACTIC Manispaa ya Songea, amesema barabara zote zenye kilomita 10.01 zimejengwa katika kata za Mjini, Misufini, Majengo na Mfaranyaki. Ameeleza kuwa utekelezaji umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2025, ambapo kazi zilizobaki ni kuweka alama za barabarani, kuziba mifereji, kuweka taa za barabarani na taa za kuongozea magari (traffic lights). Ameongeza kuwa kukamilika kwa kazi hizo kutaubadilisha kabisa mwonekano wa mji hususan nyakati za usiku.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea, Mhandisi Bakari John, ameeleza kuwa kabla ya mradi walikuwa wakitekeleza barabara za lami zenye urefu wa kilomita 2 pekee, lakini kupitia TACTIC wamefanikisha ujenzi wa kilomita 10.01. Amesema hatua hiyo imeleta matokeo makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu, kuboresha biashara na uchumi, kupunguza msongamano wa magari na kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara katika mji wa Songea.
Naye, Editha Polisa, Mtendaji wa Mtaa wa Matomondo, amesema kabla ya mradi huo barabara zilikuwa na mashimo na wakati wa mvua maji yalikuwa yanaingia kwenye nyumba za watu. Hata hivyo, baada ya mradi, hali imebadilika; uchumi umeinuka, nyumba zimepanda thamani na wananchi wanapata huduma za kijamii na kiuchumi bila vikwazo. Ameongeza kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi kuhusu kulinda miundombinu hiyo, ikiwemo kuepuka kutupa taka kwenye mitaro ili kuepusha kuziba na kuharibu barabara.
Christopher Pata, mkazi wa Songea anayejishughulisha na biashara ya chipsi, ameishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara ya lami ambayo imewasaidia kuinua uchumi wao. Ameeleza kuwa magari na bajaji sasa yanafika kirahisi na hivyo kuongeza wateja, tofauti na awali ambapo njia ilikuwa na mashimo, vumbi na matope. Ameongeza kuwa kukiwa na taa za barabarani, biashara zao zitaendelea hadi usiku bila changamoto yoyote.
Aidha, Rashid Ally, dereva wa pikipiki na mkazi wa Songea, amesema awali walikuwa wakitumia muda mrefu kuwapeleka wagonjwa hospitali ya Mjimwema kutokana na ubovu wa barabara, jambo lililosababisha vyombo vyao kuharibika mara kwa mara. Hata hivyo, baada ya barabara za lami kujengwa, usafiri umekuwa mzuri na hata nauli imeshuka kutoka shilingi 2,000 hadi kati ya shilingi 1,000 na 1,500.
Vilevile, Hassan Pili, mkazi wa Songea, ameishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja la Matarawe. Amesema hapo awali walikuwa wakipata shida kubwa kuvuka ili kufuata huduma za kijamii na kiuchumi, lakini sasa wanapita bila changamoto yoyote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED